Rombo. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, wamesema licha ya jitihada zinazoendelea za kutoa elimu kuhusu kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), bado kuna haja ya kuongeza upatikanaji wa kondomu wilayani humo kutokana na kuendelea kushamiri kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Madiwani hao wamesema baadhi ya vijana wanaojiingiza katika vitendo vya ngono hujihusisha pia na unywaji wa pombe kupita kiasi, hali inayowasahaulisha kutumia kinga wanapokutana na wenzao, jambo linalodaiwa kuchangia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Wakizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi mwishoni mwa wiki, wamesema bado kuna changamoto ya vijana kupuuza tahadhari dhidi ya Ukimwi licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Shimbi kwa Ndele, Erasmus Kiwango amesema licha ya elimu inayotolewa wilayani humo, bado upatikanaji wa kondomu ni mdogo, hivyo akataka ziongezwe na kusisitiza matumizi yake.
“Kondomu 500 ni kidogo sana, nadhani hata usiku mmoja zinaweza kuisha, ni bora tukawa na kondomu za kutosha sambamba na kutoa elimu, kwa sababu kiini cha maambukizi tunakijua na ndipo tuwekeze nguvu,” amesema Diwani Kiwango.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kirongo Samanga, Prisila Shayo, amesema pamoja na elimu kutolewa, baadhi ya vijana huipuuzia hasa wanapokuwa wamelewa na kushindwa kutumia kondomu.
“Hapa Mwenyekiti tunasema tunatoa kondomu, tukumbuke huku vijijini vijana ni walevi wakikutana na mabinti hata kutumia hiyo kondomu ni shida,”amesema diwani huyo.
Ameongeza kuwa baadhi ya vijana hudharau ugonjwa huo, huku wengine wakisema afadhali wapate Ukimwi kuliko magonjwa mengine, hali inayotokana na kutokuelewa madhara halisi ya ugonjwa huo.
Naye, Diwani wa Kata ya Katangara Mrere, Venance Mallel amesema wakati wa msimu wa mazao ya parachichi na maembe, baadhi ya vijana huingia kwenye vitendo vya uasherati baada ya kupata fedha, jambo linalochochea maambukizi hayo.
“Tarafa ya Mashati, wakati wa msimu wa kuuza parachichi na maembe, vijana wakishapata fedha huishia kwenye anasa na ulevi, hivyo maambukizi ya magonjwa yanaongezeka,” amesema Diwani Mallel.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ubetu Kahe, Mzee Longela, amesema, “Hili suala la Ukimwi sio la mzaha. Tunapaswa kutoa elimu ya kutosha, ikiwemo kwenye baa ili hata wahudumu waelewe hatari ya tatizo hili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Gilbert Tarimo, amesema takwimu za afya za Novemba 2025 zinaonyesha kuwa wanawake wanachangia asilimia nane ya maambukizi ya VVU/Ukimwi huku wanaume wakiwa ni asilimia saba.
“Hii inaonyesha kuwa badala ya maambukizi kupungua, yanaongezeka. Hivyo ni lazima kuchukua hatua madhubuti,” amesema Tarimo.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana, Halmashauri iligawa kondomu 500 sambamba na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Godwin Chacha, amewataka madiwani kutumia vikao vya kata kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda afya zao na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa kwa wakati.