Shauri kupinga Tume ya Jaji Chande kusikilizwa Februari 26

Dar es Salaam. Wakati Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya  Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ikikaribia kumaliza kazi yake, Mahakama Kuu imepanga kusikiliza shauri la kupinga uhalali wa tume hiyo Februari 26, 2026.

Tarehe hiyo ya usikilizwaji wa shauri hilo imepangwa na Jaji Awamu Mbagwa anayelisikiliza wakati lilipotajwa leo Februari 10, 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kwa ajili ya amri muhimu za Mahakama.

Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 nchini kuliibuka  vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi, vifo na majeruhi, kufuatia maandamano ya  kupinga uchaguzi huo katika majiji na miji mbalimbali nchini.

Kufuatia matukio hayo, Novemba 18, 2025  Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo, wakati na baada ya uchaguzi, inayoongozwa Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande na akaizindua Novemba 20, 2025, huku akiipa miezi mitatu kukamilisha jukumu hilo.

Hata hivyo, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Mahinyila, wamefungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake, baada ya kupata ridhaa ya mahakama hiyo.

Wajibu maombi wengine ni Jaji Mkuu mstaafu, Chande (mwenyekiti wa tume hiyo) na wajumbe, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema.

Wengine ni Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Dk Stergomena Tax na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Kwa mujibu wa waombaji, TLS kilichoundwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge,  majukumu yake ya msingi ni pamoja na kukuza utawala wa sheria, uadilifu na uwazi, kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusu sheria.

Wakati shauri hilo lilipotajwa leo Mahakama imewapa siku saba kuanzia leo wajibu maombi wote kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao dhidi ya madai ya wadai kabla ya tarehe hiyo ya usikilizwaji.

Tarehe hiyo ndio Mahakama itasikiliza hoja za msingi za waombaji za kuipinga tume hiyo ambapo kupitia mawakili wao watatoa ufafanuzi wa kina wa sababu zao kuipinga tume hiyo kabla ya wajibu maombi nao kujibu hoja za waombaji.

Baada ya kukamilisha usikilizwaji huo Mahakama itapanga tarehe kwa ajili ya uamuzi wake.

Katika shauri hilo waombaji hao ambao wanawakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu wanaiomba mahakama hiyo itoe amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.

Wanadai kuwa tume hiyo haijakidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa uundwaji na uteuzi wa wajumbe wake ulifanywa kwa nia ovu kinyume cha kanuni ya haki asili ya mtu kutokuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.

Wanafafanua hoja hiyo kuwa kwanza, mamlaka ya uteuzi ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, na kwa hivyo kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo.

Pia, wanadai kuwa mjumbe Dk Tax ni mtuhumiwa kwani alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.

Vilevile wanadai kuwa majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu hizo kwani baadhi ya mali zilizoharibiwa ni za Mahakama waliyoiongoza, na IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.

Wanaongeza kuwa Amiri Jeshi Mkuu, mamlaka ya uteuzi wa tume hiyo (Rais) katika tarehe tofautitofauti alitoa maagizo kwa Polisi na Jeshi kujiandaa kwa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi.

Katika hoja nyingine wanadai kuwa uundaji wa tume hiyo umekiuka masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023, kifungu cha 16.

Wakifafanua hoja hiyo wanadai  kuwa hakuna ufafanuzi wa madhumuni yake yaliyo wazi kama kifungu hicho kinaielekeza mamlaka ya uteuzi  bali  yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba, utawala bora na utaratibu sahihi wa haki.

Pia, wanadai maneno yaliyotumika ‘uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani’ yanapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.

Hoja nyingine wanadai kuwa Tume hiyo si huru. Wanafafanua kuwa  haikujumuisha wajumbe kutoka vyama huru vya kitaaluma kama TLS, Chama cha madaktari, mashirika ya kijamii, ya kidini kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) au wadau wengine huru wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka  upendeleo kwa mamlaka ya uteuzi.

Wanadai wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa.

Hivyo, wanadai wajumbe hao hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao.