Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu wa familia moja, Solomon Mwambyale na watoto wake wawili Stephano Mwaisango na Emanuel Mwaisango kwa tuhuma za mauaji ya Jenti Sengela (87) ambaye alikuwa shemeji wa mtuhumiwa Solomon Mwambyale.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Februari 7, 2026 katika Kitongoji cha Busoka Kijiji cha Lusungo Kata ya Makwale, ambapo inadaiwa mtuhumiwa kwa kushirikiana na watoto wake walimuua Jenti kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kisha kukimbia.
Taarifa iliyotolewa leo Februari 10,2026 na Jeshi la Polisi mkoani humo, imeeleza kuwa kupitia askari wa kuchunguza matukio ya mauaji walianza msako na Februari 8,2026 walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mashamba ya ukoo na tamaa ya kujipatia mali kwa njia isiyo sahihi, watuhumiwa wote walikamatwa saa 7 usiku,”imeeleza taarifa hiyo.
Wakati huohuo, Jeshi hilo linawashikilia watu wanne akiwamo mwanafunzi wa Chuo Kikuu Iringa, Wilfred Komba kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 45 na gramu 785.
Wengine waliokamatwa ni Lenard Shamba ‘Paulo’ mkazi wa Tarime, James Mwakalebela mkazi wa Kyela na Joseph Mkwara ‘Aliki’ mkazi wa Kyela mkoani Mbeya, ambapo uchunguzi umebaini kuwa waliingiza dawa hizo kutoka nchi jirani.
“Watuhumiwa walikamatwa na dawa hizo zikiwa kwenye mabegi matatu na mifuko miwili ya sandalusi wakizisafirisha kwa mabasi ya abiria kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam,” imeeleza taarifa ya Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga.
Pia, Jeshi hilo linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuingilia mfumo wa kibiashara wa kampuni za ukopeshaji simu, ambao ni Charles Oden ’Mwakasege’ na Isack Charles ambaye ni fundi simu mkazi wa Meta jijini Mbeya.
“Watuhumiwa walikamatwa kwenye msako uliofanyika Januari 27 hadi Februari 5 mwaka huu katika mtaa wa Rungwe Music Mwanjelwa jijini Mbeya, inadaiwa wamekuwa wakibadili simu zilizokopwa na watu.
“Wanaondoa mfumo uliowekwa ili waliokopeshwa wasiweze kufuatiliwa katika kulipa deni kupitia kampuni zilizowakopesha, baada ya upekuzi watuhumiwa walikutwa na simu za Samsung, Infinix, Tecno, Itel na Yas 1,” imeeleza taarifa hiyo.