Dar es Salaam. Kesi ya kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe na mwenzake, imehamishiwa kwa hakimu mwingine na sasa itaendelea kesho kwa ajili ya kusikilizwa.
Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Meneja na Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake.
Kwa upande wa mshtakiwa John, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.
Leo Jumanne Februari 10, 2026 kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa Jamhuri, lakini washtakiwa hao walipofika mahakamani, walielezwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhini kuwa kesi hiyo imehamishiwa kwake.
Hakimu Mhini alisema kutokana na kesi hiyo kuhamishiwa kwake, inabidi apitie jalada la kesi hiyo kabla ya kuendelea na usikilizwaji.
“Washtakiwa kwa kuwa kesi yenu imehamishiwa kwangu, inabidi nilipitie jalada la kesi hii kabla ya kuendelea na kwa sababu hiyo naiahirisha kesi hii hadi kesho itakapoendelea na usikilizwaji wa mashahidi,” amesema Hakimu Mhini
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali Erick Mabagala, ameieleza mahakama kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji na leo wana mashahidi wawili na wapo tayari kuendelea usikilizwaji.
Awali, kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki na sasa itakuwa mbele ya hakimu Mhini
Tayari mashahidi 10 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.
Katika mashtaka hayo 126, 117 ni ya kuendesha biashara ya upatu yanayowakabili washtakiwa wote wawili na mashtaka tisa ni ya kutakatisha yanayomkabili Mkondya pekee yake.
Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.
Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Meneja wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia pesa kutoka kwa watu zaidi ya 117 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya peke yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.
Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.