Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kutoa elimu/mafunzo kwa Vyuo vikuu pamoja na Shule za Sekondari ikiwa na lengo la kuwajengea ufahamu kuhusu shughuli mbalimbali za Bodi na kukuza taaluma ya Uhasibu.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA CPA Pius Maneno amekipongeza chuo hicho kwa kuwa na mwendelezo wa kuwaleta wanachuo wanaosoma masomo ya Uhasibu na Biashara kwenye Bodi hiyo ili kupata elimu kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi.
Malendeja amesema ili kuwa Mhasibu au Mkaguzi inabidi kufanya mitihani ya Bodi hiyo ili kupewa cheti cha kitaaluma ili uweze kutambulika kisheria kama Mhasibu au Mkaguzi ambapo cheti hicho kitakutambulisha kitaifa na kimataifa na kuweza kufanya kazi nje na ndani ya nchi.
“Nimefarijika kuona wanafunzi wa Sheria pia wakishiriki katika ziara hii na kupata mafunzo kwani wana nafasi ya kusomea masomo ya Uhasibu na kuwa CPA yaani “Certified Public Accountant” alisema Malendeja
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya amesema ziara hiyo imekuwa chachu kwa wanafunzi kwani wanapata taarifa mbalimbali kuhusu NBAA
Aliongeza kuwa kupitia matukio mbalimbali NBAA husikiliza maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu huduma zake kwa mfano NBAA imesikia kilio cha wadau wake kuhusu ucheleweshwaji wa vyeti vya Kitaaluma kwa kuomba Bodi kusaidia upatikanaji wa vyeti mapema wanapomaliza na sio kwa kusubiri kwa muda mrefu. Na sasa NBAA imeamua kuanzisha Mahafali nyingine ili kukidhi mahitaji ya wadau wake, na kwa mara ya kwanza mahafali hayo yatafanyika tarehe 28 Machi, 2026 katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam. Maana yake kwa mwaka kutakuwa na mahafali mbili yaani Machi na Septemba au Oktoba mwanzoni.