KATIKA muendelezo wa kujenga kikosi cha Simba mabosi wa klabu hiyo hivi karibuni walimshusha winga Anicet Oura ambaye tayari ameshaonyesha makali kwenye michezo mitatu, mmoja wa Ligi Kuu pamoja na miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kocha wa ASEC Mimosas Julien Chevalier, amesema Wekundu hao wamepata jembe.
Simba imemsajili kiungo huyo raia wa Ivory Coasta kwenye dirisha dogo la usajili akitokea Gnistan ambapo tayari ameshaonyesha makali yake uwanjani na mashabiki wameanza kuamini kwenye kiwango chake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Julien ambaye aliwahi kutakiwa na Yanga amesema Simba imepata winga wa shoka kwani ni miongoni mwa wachezaji bora aliowahi kuwaona ndani ya Ivory Coast.
Amesema kuwa Oura ni winga mzuri ambaye kama akiunganika vyema na wenzake na wakapata washambuliaji bora basi Simba itapata mabao mengi.
“Sifa ya kwanza ya Oura ni mchezaji mbunifu sana, lakini bahati mbaya walichelewa kumpata kama angeanza mapema msimu huu angewasaidia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa.
“Wakati ambao Oura alikuwa ASEC alikuwa akipigiwa hesabu na klabu nyingi za Ulaya kutokana na ubora wake ila ilishindikana kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
“Ila naamini akipata muda atakuwa hatari zaidi, jambo zuri ameenda kwenye timu ambayo ina mashabiki wengi na inajitengeneza upya, jambo zuri zaidi anafanya kazi na kocha wanaofahamiana,” amesema kocha huyo.
Ikumbukwe kuwa, Oura ni chaguo la kocha Steven Barker ili aweze kuongeza nguvu katika eneo hilo ambalo linachezewa na mastaa wengine akiwemo Elie Mpanzu.
Oura (26) ambaye amewahi kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ivory Coast aliwahi kuichezea ASEC msimu wa 2021/2022, kabla ya kutimkia Stellenbosch ambayo ilikuwa ikinolewa na kocha Barker ambapo alichezea ndani ya mwaka mmoja na kufunga mabao manne.
Mpaka sasa Simba imeshapoteza matumaini ya kuendelea na hatua inayofuata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imekusanya pointi mbili tu kwenye michezo mitano na wikiendi ijayo itakamilisha michezo ya makundi kwa kuvaana na Stade Malien ambayo imeshafuzu robo fainali ikiwa na pointi 11.