Kenyatta anavyoujenga upya muungano wa Azimio kumkabili Ruto 2027

Hatua ya kushtukiza ya Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ya kuanzisha mchakato wa kuufanyia mageuzi muungano wa Azimio la Umoja ili kuunda upinzani wenye umoja dhidi ya Rais William Ruto, imeongeza msisimko mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Kenyatta, anayefahamika kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha, anadaiwa kupanga kuufadhili muungano huo pamoja na kuwavuta wanasiasa wote wanaopinga kurejea kwa Ruto Ikulu kwa muhula mwingine wa miaka mitano, wakiwemo waasi wa ODM.

Sehemu nyingine ya mpango huo ni kuwahusisha wafanyabiashara wakubwa na wenye uwezo wa kifedha ili kugharamia kampeni. Kenyatta alikuwa mhimili mkuu wa kuundwa kwa Azimio, muungano uliomsimamisha Raila Odinga bila mafanikio katika uchaguzi wa 2022 dhidi ya Ruto wa UDA.

Baada ya hapo, muungano huo uliingia usingizini kufuatia ODM kuamua kushirikiana na UDA katika kile kilichoelezwa kuwa serikali ya mseto.

Gazeti la Nation limepata taarifa za kikao kilichoongozwa na Uhuru Jumatatu iliyopita katika Kituo cha SKM, Karen, Nairobi, ambacho tangu hapo kimeanza kuratibu shughuli muhimu, zikiwemo kushinikiza mabadiliko ya uongozi katika kambi ya wachache bungeni na kufikia mitandao ya kisiasa ya marehemu Odinga.

Wazo kuu ni kwamba wafuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Odinga, bado wanaweza kujitambulisha kama Azimio katika uchaguzi ujao, huku muungano huo ukiendelea kujadiliana na wadau wengine wa kisiasa, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais, Rigathi Gachagua wa chama cha DCP ili kupanua wigo wa uungwaji mkono.

Inadaiwa Kenyatta anafanya kila awezalo kuhakikisha upinzani unakuwa na mgombea mmoja wa urais ili kuepuka kurudia kosa la uchaguzi wa kihistoria wa mwaka 1992 ambapo upinzani ulisambaratika kwa kusimamisha wagombea wengi na kumpa Rais wa wakati huo, Daniel arap Moi, ushindi mwingine wakati nchi ilionekana kuwa tayari kwa mabadiliko.

Kikao hicho kiliongozwa na Kenyatta kwa njia ya mtandao. Waliohudhuria ni pamoja na Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Narc na aliyekuwa Gavana wa Kitui, Charity Ngilu, Mkurugenzi Mtendaji wa Azimio anayeondoka Raphael Tuju, Katibu Mkuu wa Jubilee, Moitalel ole Kenta, Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, Makamu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe na Seneta wa Kitui, Enoch Wambua.

Hata hivyo, ODM chama kikubwa zaidi ndani ya Muungano wa Azimio, kimekataa mabadiliko hayo.

Baada ya kikao, Kalonzo Musyoka aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Azimio akimrithi marehemu Raila Odinga, hatua inayolenga kuongeza mvuto wa kisiasa wa kiongozi huyo wa Wiper na kuupa nguvu zaidi mkakati wa kumzuia Ruto kutawala kwa zaidi ya muhula mmoja.

Licha ya hofu za awali kuwa Gachagua angepinga msimamo mkali wa Kenyatta na kufufuliwa kwa muungano uliokuwa umedorora, aliyekuwa makamu wa rais ameonekana kuchagua kutotikisa jahazi.

“Chama cha DCP kinampongeza Kalonzo Musyoka kwa kuteuliwa na kukubali kuwa Kiongozi wa Chama cha Muungano wa Azimio La Umoja. Hatua hii ya ujasiri iliyochukuliwa na mwenyekiti, Rais Uhuru Kenyatta, uongozi wa muungano na vyama vyote ni mwelekeo sahihi kuelekea siku zijazo huku kuzaliwa upya kwa Taifa letu kukitarajiwa Agosti 10, 2027.

“Tunasonga mbele kwa mshikamano na tukiwa tumejikita katika masilahi mapana ya Taifa,” alisema Gachagua.

Uhuru sasa amejiweka katika nafasi ya msimamizi mkuu wa mikakati ya kisiasa, akilenga kumwangusha mrithi wake aliyekuwa makamu wake kwa miaka 10 alipokuwa na udhibiti wa vyombo vya dola.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema hakuna muungano wa kisiasa nchini Kenya uliowahi kudumu zaidi ya mzunguko mmoja wa uchaguzi, hali inayofanya mpango wa Uhuru uonekane kwa macho ya wasiwasi.

Kiongozi wa Kanu, Gideon Moi, aliwakilishwa katika kikao hicho na Tony Gachoka, aliyeliambia Nation kuwa mkakati wa Uhuru ni kwanza kuunganisha washirika wa Azimio kabla ya kujadiliana na washirika wengine wa kisiasa.

Kikao hicho pia kilitenga dakika moja ya ukimya kumuenzi marehemu Odinga, huku Kenyatta akiongoza ujumbe wa heshima na tafakari juu ya urithi wa mwanasiasa huyo mkongwe.

“Kenyatta alikuwa akitekeleza wajibu wake kama mwenyekiti wa baraza la muungano. Aliitisha kikao hicho kwa lengo la kumpata kiongozi atakayemrithi marehemu Odinga,” alisema Msemaji wa Kenyatta, Kanze Dena.

Aliongeza: “Kalonzo sasa atakuwa msimamizi wa shughuli zote za muungano, ikiwemo mipango ya baadaye na maandalizi ya uchaguzi.”

Akizungumza katika mahojiano maalumu, mbunge Caroli Omondi alisema kikao hicho kiliitishwa baada ya mashauriano mapana yaliyohusisha familia ya Odinga na mitandao yake ya zamani ya kisiasa.

Alisema: “Upinzani ulioungana na kuratibiwa vyema utamshinda Ruto kwa tofauti ya karibu kura milioni tano.”

Hata hivyo, Nation haikuweza kuthibitisha kwa uhuru ushiriki wa familia ya Odinga katika mpango huo. Lakini binti yake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Winnie Odinga, amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya mseto na mazungumzo ya muungano kati ya ODM na UDA.

Kwa mtazamo mpana, Kenyatta na mikakati yake inalenga kuipa Azimio sura mpya ili ivutie zaidi vijana (Gen Z) pamoja na washirika wapya. Pia, kuna mipango ya kuwafikia baadhi ya washirika waliokuwa wamejiondoa rasmi katika muungano huo.

“Iliafikiwa kuwa milango ifunguliwe kwa wanaotaka kujiunga. Pia, tulikubaliana muungano ufanyiwe mageuzi ili kuwavutia vijana na makundi mengine ya upinzani yaliyoungana. Sehemu ya mageuzi ni kuruhusu wanachama kujiunga kama watu binafsi au kupitia vyama vingine. Azimio itaamua mpangilio wa Bunge,” alisema Omondi.

Inadaiwa pia kikao kilijadili namna ya kunufaika na mgawanyiko ndani ya ODM kwa kuruhusu wanachama wasioridhika kujiunga na Azimio kama watu binafsi na kugombea kwa tiketi yake. Katika uchaguzi wa 2022, Raila na mgombea mwenza wake Martha Karua pekee ndio waligombea kwa tiketi ya muungano, huku wagombea wengine wakitumia vyama tanzu.

Omondi alibainisha kuwa mkakati ni kuwakusanya tena watu waliowahi kufanya kazi na Raila katika chaguzi zilizopita, kwa lengo la kutumia Azimio kulinda ngome zake za jadi za kisiasa.