Kitu kikubwa ambacho wazee wetu hawakukijua, kwenye michezo yetu ya utotoni tuliigiza tabia za baba zetu.
Mtoto wa mfanyakazi aliigiza kama mfanyakazi, kadhalika wa mkulima pia aliigiza hivyo.
Sipati picha kama mlevi angegundua kuwa mwanaye anamuigiza hadharani kwenye michezo. Bila shaka mtoto huyo angekiona kilichomtoa nyoka miguu, na si ajabu ungelikuwa ndio mwisho wake kucheza.
Lakini sisi tulienda mbali zaidi. Mtoto wa daktari aliigiza kama daktari. Angewapita “wagonjwa” walioketi latila foleni na kujifungia ofisini.
Baada ya dakika kadhaa angegonga kengele kumruhusu mtoto wa kwanza aliyeigiza kama mgonjwa: “Toa ulimi, kohoa kidogo” kisha akamkagua macho. Akachukua karatasi na kucharaza vitu visivyoeleweka juu yake.
Kisha akabonyeza kengele kumwita ‘mgonjwa’ aliyefuata.
Ukiachilia mbali madaktari, tulikuwa na kada zote katika michezo yetu. Kulikuwa na walimu, madereva, maaskari na kadhalika.
Tulikuwa tukicheza bila kujua kuwa tulikuwa tukijenga uzoefu wa baadaye. Na kweli kuna waliofanikiwa kuunganisha michezo hiyo na masomo yao, wakatokea kuwa wafanyakazi bora sana katika kada zao.
Kila anayekutana nao anakiri kuwa watu hawa wana wito katika kazi zao. Viongozi bora pia walitokea huko.
Tulikuwa na viongozi tofauti waliowaiga wajumbe wa nyumba kumi, na viongozi wengine waliopata kututembelea kitongojini.
Walikuwapo watoto walioigiza kama viongozi waadilifu, lakini wengine wakawaiga viongozi wazembe na wasio na weledi. Kufuatia tofauti hizo, wapo waliopandishwa vyeo na wengine kufukuzwa kazi. Kwa ujumla tuliakisi maisha ya jamii nzima kwenye michezo kwa kadiri tulivyoyaona.
Kama vile tulivyojikaririsha kuwa “ualimu ni wito”, ndivyo ilivyo kwenye kila kada au fani.
Muuguzi anayefanya kazi vizuri ni yule mwenye wito kwenye kazi hiyo. Lakini pia kiongozi mzuri ni yule aliye na wito katika nafasi yake. Mengi yanakuja kujitokeza huko mbeleni, lakini kwanza ni wito. Akiwa na wito ndio anaweza kujiendeleza hata akawa mbobezi kwenye eneo lake. Lakini akikosa wito hatafika popote.
Mara nyingi tunasoma sifa za viongozi wetu walio wengi, tunaona kuwa kabla ya kufikia walipo walichipukia tangu wakiwa kwenye shule za awali.
Walimudu kushikilia bomba la uongozi hadi kwenye shule za upili na vyuoni kabla ya kujitokeza kwenye jamii. Kiongozi wa aina hii ni aghalabu kufanya makosa ya kitoto, kwani alishanyoshana na watoto wenzake tangu utotoni. Hakuna mambo mapya yanayoweza kumuondoa kwenye mstari.
Mara nyingi tofauti kwake inakuwa ni mifumo ya uongozi kulingana na Serikali anayoitumikia.
Kwanza Inambidi awe mbunifu anayetatua matatizo ya watu kisayansi. Lakini hapaswi kwenda tofauti na dira na sera zilizowekwa na Serikali yake.
Awapo mgeni kwenye safu ya uongozi, hana budi kujifunza mafanikio na maanguko ya viongozi waliomtangulia.
Hii itamwepusha kurudia makosa yaliyofanywa na watangulizi wake.
Viongozi wengi wageni wamekuwa wepesi wa kuwaiga wakubwa wao katika kutoa maamuzi. Kwa mfano kauli ya Waziri Mkuu kwamba wakandarasi wazembe wasivumiliwe inatekelezwa kwa nguvu sana.
Tumesikia huku na huko wakuu wa Mikoa na Wilaya wakiwafurumusha wakandarasi kuondoka kwenye miradi. Kwa upande mmoja ni safi sana, kwa kuwa Serikali inaonesha kuwa ipo makini kwenye maendeleo ya watu wake.
Lakini angalizo kwa wakuu hao, wasije kujisahau na kupitiliza. Kwenye maadhimisho ya siku ya sheria duniani, Mwenyekiti wa chama cha wanasheria aliasa jambo muhimu sana. Alisema maamuzi na maagizo ya viongozi yasisigane na sheria.
Nafikiri aliyasema hayo baada ya matukio yaliyowahi kujitokeza. Katika maeneo na nyakati tofauti, wakuu fulani waliwatumbua na hata kuwaweka ndani baadhi ya watu waliodaiwa kufanya uzembe.
Nadhani hii ni tahadhari kwamba pelege aliyemla dagaa, anaweza naye akaingia mdomoni mwa chewa. Kwa kuwa wakuu hao wana wakubwa wao katika chama, wasije nao wakaja kuingia kwenye kumi na nane za viongozi wa chama.
Nasema hivyo baada ya kuona kasi ya watendaji wa chama kwenye miradi ya maendeleo. Ni kama vile ile kaulimbiu ya “Chama Kimeshika Hatamu” imerejea kimtindo.
Kauli hii ilikuwa maarufu sana enzi ya chama kimoja. Ikaja kupungua nguvu kama siyo kuachwa baada ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuzinduliwa nchini. Katika mfumo ule, wanasiasa kutoka kwenye chama walikuwa na sauti kubwa kwenye Mashirika ya Umma.
Walikuwa juu ya wataalamu wa fani mbalimbali. Lakini kwa bahati mbaya walikuwa wakiendesha kazi kisiasa.
Hii inawezekana kuwa ndiyo iliyodhoofisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwa kuwa mtaji wa wanasiasa ni wananchi, nao watataka kujionesha kwa wananchi kupitia uzalishaji. Kwamba bila wao maendeleo hayawezekani. Tusishangae wataalamu kutoka vyama pinzani wakiwekwa kando. Mbaya zaidi hivi sasa tuna viongozi wengi wanaojihusisha na biashara. Kama tukiyaacha haya yafanyike bila utaratibu maalum, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea migongano ya kimaslahi.
Bila usimamizi thabiti wa Serikali, upinzani wa kiitikadi unaweza kuathiri maendeleo.
Maombi ya tenda za utekelezaji wa miradi yanaweza kuangaliwa kwa vigezo vya itikadi badala ya utaalamu.
Ni mwanachama yupi wa Simba anayefurahia ushindi wa Yanga? Badala yake mtu atajiuliza: “Kwa nini nimpe faida mtu asiye upande wangu?” Tukifika hapo tutakuwa tumefeli.