FYATU MFYATUZI: Fyatu kwenda Romu kumuombea Popu aanze kuwaombea Mafyatu

Mwenzenu napanga kwenda Vatikano kukutana na popu kumuomba na kumuombea aombee amani. Nitaadamana na baadhi ya mashehena sorry mashehu wenzangu. Tutahakikisha anaombea amani tu bila haki.

Naona yule anashaangaa akadhani mibangi imenifyatua nikafyatuka na kutaka kuifyatua amani! Nina sababu nzuri tu za amani tena kwa amani. Baada ya mafyatu kuzidisha ufyatu hadi kutaka haki kwa gharama ya amani, kama mhimili mkuu wa amani Fyatuland, naanza kushindwa kuwafyatua walipofyatuka wanifyatue, na mwisho wa siku, amani itoweke.

Sipendi niwafanyie kitu mbaya wakose amani na kunilazimisha kukimbilia kutafuta moto kwenya maji kama suluhu kama yule sulubu. Mpango mzima ni kuikomboa Fyatuland isijiangamize kwa ufyatu. Nikifika, nitamsihi sana aombe mafyatu wawe na amani katika kila jambo. Mfano, wakifyatuliwa, wawe na amani.Wakiburuzwa, wawe na amani.

Nitamuomba na kumuombea popu aombe amani ili mafyatu, hata wakipigwa au kupigana, wafanye hivyo kwa amani, watulize boli wawe na amani. Maana, bila amani, itakuwa vigumu kuishi na kufyatuana. Amani ni uhai na uhai ni amani; haki ni vurugu iletayo machafuko itokanayo na mafyatu kutaka wapewe hata wasivyostahili kama kujua namna ninavyowafyatua.

Najua popu atanielewa na kukubali ombi langu la kumuomba, kumuombea, aombee amani kwa amani. Nitafanya hivi kwa amani ili iwepo amani baina yetu. Nitamuomba na kumuombea aombe amani ili tuishi kwa amani bila kukwaruzana na kudaiana haki tena bila amani. Haki inaweza kuua Fyatuland kwa ukosefu amani. Uwepo wa amani utawezesha hata mvua kunyesha. Kutamalaki kwa amani kutawezesha ulaji wangu uwe na amani kiasi cha kufyatua kwa amani.

Nitamsisitizia Bwana Mkubwa kuwa amani ni tunu ambayo niko tayari kuteka, kupoteza, hata kuua kwa ajili yake. Nataka niwe na amani ya kufyatua mafyatu ila wasiwe na haki ya kunihoji, kunituhumu, kunishitaki wala kunidai au kuwa na haki ya kuvuruga amani. Mafyatu wakiwa na amani, kila kitu kitakwenda vizuri. Hapatakuwapo madai ya kipuuzi kama vile kukinukisha, kuandamana, au kulalamika. Amani haitaki mambo haya. Nataka mafyatu wawe na amani kama kondoo. Kondoo ukimchinja kwa amani, anakufa kwa amani nawe unamla kwa amani.

Kwa wasiojua haki na madhara yake, wanapenda sana kuomba na kuitaka. Haki ya nini wakati kuna amani hata kama ni ya imani? Haki inaweza kuleta machafuko.

Nani anataka haki wakati haki haileti amani bali shari? Ukitaka kuepuka machafuko, basi omba amani tena kwa sana huku ukiikataa haki. Kama utaomba haki, basi omba haki isiwepo bila amani. Maana, bila amani, hata iwepo haki, tutavurugana na kufyatuana. Nitamuombea na kumuomba popu aombe tuwe na amani ya kuwafyatua wanaotaka haki tena kwa amani. Pia, nitamuomba aombe watakaofyatuliwa watulie kwa amani ili wasivuruge amani. Nitamsisitizia aombee Fyatuland iwe na amani na kuchukia na kuepuka haki.

Nitamshauri asiombe haki. Kwani, haki huvuruga amani. Haki huwapa haki mafyatu kuvuruga amani kwa kisingizio cha kuomba na kutaka haki. Amani ni muhimu kuliko haki. Kukitamalaki amani, kila fyatu anafanya na kufyatua kila atakacho kwa amani.

Nitamuomba na kumuombea popu aombe amani kwa mafyatu waishi na kukubali kila jambo kwa amani. Wakifyatuana hata kuuana, wafanye hivyo kwa amani. Wakitekana au kupotezana, wafanye hivyo kwa amani. Watakaouawa au kufa, wafanye hivyo kwa amani. Wakizikana au kutopata maiti za waliofyatuliwa kwa sababu ya kiherehere cha kutafuta na kutaka haki, wafanye hivyo kwa amani.

Mbona kuku wana amani japo hawana haki? Kama haki ni mali basi amani ni pepo. Hivyo, nawasihi mafyatu watafute amani. Haki wataikuta mbinguni. Waombe amani ili kila kitu kifanyike kwa amani.

Kutokana kutokea mafyatu kama wale wa TEKI tena wanaojifanya wanamfuata popu kutaka kuvuruga amani kwa kudai haki, nitamuomba popu awaombee na kuwakataza kufanya hivyo kwa amani. Nitamshauri awaamuru wote wahubiri amani wakati wakijitenga na haki.

Juzi, nilikwenda baa na kufanya vurugu kwa amani. Si waliitwa ndata wanidake kwa amani. Nawashukuru sana. Hawakunikamata kwa haki bali kwa amani.

Walinipa kipigo cha amani hadi nikalalamika kwa amani. Baada ya hapo, walinifungulia kesi kwa amani. Sasa nangoja kuadhibiwa kwa amani.

Najua pilato atanipiga mvua si kidogo kwa amani. Kabla ya kufanya hivyo, nitamuomba nijitetee kwa amani ili hata nikifungwa, nifungwe kwa amani.

Nitamuomba pilato atoe amri kwa majamaa wa lupango wanifunge kwa amani. Hata pale pilato atakapotamka mvua nitakazokwenda kutumika lupango, nitamuomba atoe hukumu kwa amani.

Nitajitetea kuwa nilipofanya vurugu, kwanza, nilikata kalaji kwa amani nako kakanifyatua kwa amani kiasi cha kufanya vurugu kwa amani hadi nikakamatwa, kuhukumiwa, na kufungwa kwa amani. Kuanzia leo, Fyatuland itaitwa amani na itakuwa mwiko kwa fyatu yeyote kutuletea makelele haki. Du! Majinamizi mengine, acha tu! Inaonekana mgoshi Machungi keshanipiga zongo.