Matajiri wakubwa wa ulimwengu, wanasiasa wenye nguvu kubwa ya ushawishi na wanaoweza kutengeneza matokeo (movers and shakers), maji hayashuki, chakula hakiteremki, sababu ikiwa hatima ya yaliyomo ndani ya Mafaili ya Epstein.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ni mmoja wa watajwa kwenye maudhui ya Mafaili ya Epstein. Kampeni za urais mwaka 2024, Trump aliahidi kwa kishindo kuwa angeacha wazi Mafaili ya Epstein kama angeshinda. Kumbe alikuwa akijikaanga kwa mafuta yake mwenyewe.
Baada ya kushinda kiti, Trump alipuuzia ahadi yake ya Mafaili ya Epstein, akadai kuwa hoja tajwa ni uzushi wa chama pinzani, Democratic, ikichochewa na mahasimu wake, Joe Biden, Barack Obama na Hillary Clinton.
Mafaili ya Epstein ni nyaraka zenye kurasa milioni sita, vilevile picha mnato, video na barua pepe, vikibeba ushahidi wa matukio ya uhalifu wa kingono dhidi ya watoto, uliotekelezwa na mhalifu wa ngono, Jeffrey Epstein, na wenzake.
Epstein, alifariki dunia Agosti 10, 2019, akiwa kwenye jela maalum, ndani ya Gereza la Metropolitan Correction Centre (MCC), New York, Marekani. Ripoti ya kitabibu ilieleza kuwa alijiua. Mazingira ya kifo yalitengeneza wasiwasi mkubwa kwamba aliuawa kuficha siri za wakubwa.
Mzawa wa Brooklyn, New York, Marekani. Wazazi wa Epstein, Seymour George Epstein (baba) na Pauline “Paula” Stolofsky (mama), ni Wayahudi waliohamia Marekani. Epstein ni kaka mkubwa katika uzao wa watoto watatu.
Mkusanyiko wa taarifa za Epstein, unampambanua Mmarekani-Myahudi huyo kuwa tapeli wa kimataifa, na mhalifu wa ngono. Aliwatumikisha watoto kingono, alifanya usafirishaji wa binadamu (human trafficking), vilevile kuwaunganisha watu na watoto kingono.
Kwa miaka mingi, hasa baada ya kifo chake, kumekuwa na uvumi mkubwa kwamba Epstein alitunza ushahidi wa kila mteja wake, aliyemuunganisha kushiriki ngono na watoto. Wateja wake ni watu wazito, matajiri wakubwa na wanasiasa mashuhuri.
Uvumi huo ndiyo ambao umejenga dhana kwenye uso wa jamii kwamba Epstein aliuawa mahabusu Agosti 2019, ili kuficha siri za watu wasioguswa (untouchables). Ni kuanzia wakati huo kumekuwa na shinikizo la Mafaili ya Epstein kuachwa wazi mbele ya macho na masikio ya umma.
Ripoti za maisha yake ya mwanzo, zinamtaja Epstein kama mtu mwenye akili, aliyefanya vema kwenye somo la Hisabati na alikuwa na kipaji cha muziki. Epstein alijifunza na kuwa hodari wa kuchezea piano. Muziki hakuupa nafasi, ila Hisabati ilimfikisha mbali, ingawa si kwa njia halali.
Alianza kusoma shule ya chipukizi ya Mark Twain, ambayo inasimamiwa na Idara ya Elimu ya Jiji la New York (NYCDOE). Kutokana na uwezo wake wa kunasa masomo haraka, Epstein alikuwa akilipwa na wanafunzi wenzake ili awafundishe katika muda wa ziada.
Mwaka 1967, Epstein alijiunga na Kituo cha Sanaa cha Interlochen, kwa ajili ya kujinoa zaidi kimuziki. Mwaka 1969, alihitimu elimu ya juu, Shule ya Lafayette, iliyopo Brooklyn, New York. Mwaka 1971, alijiunga na Chuo cha Cooper Union, kilichopo Manhattan, New York, kwa ajili ya kusoma Hisabati, lakini alisoma kwa miezi michache.
Septemba 1971, Epstein alidahiliwa kwenye Taasisi ya Sayansi ya Hisabati ya Courant, Chuo Kikuu cha New York. Juni 1974, Epstein aliacha chuo kabla hajahitimu shahada yake. Baada ya hapo alianza kufanya kazi ya ualimu. Shule aliyojiunga nayo kama mwalimu ni Dalton, iliyopo Manhattan, New York.
Ni kipindi hiki cha ualimu, ndicho alianza kuonesha tabia isiyofaa kwa watoto wa kike. Alipenda sana kujenga nao ukaribu, zaidi alihudhuria matukio ya sherehe za watoto wa kike, hasa zile ambazo zilikuwa na pombe.
Dalton ni shule ambayo watoto wawili wa Alan Greenberg, walikuwa wakisoma. Greenberg alikiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi kubwa ya kifedha ya Bear Stearns. Mtoto wa kike wa Greenberg, ndiye aliyemtambulisha Epstein kwa baba yake. Baada ya hapo, Greenberg na Epstein wakawa marafiki.
Mwaka 1976, Epstein aliachishwa kazi Dalton, moja kwa moja Greenberg alimwajiri Bear Stearns, kama mfanyakazi wa chini. Uwezo wake kazini ulimfanya apande ngazi hadi kuwa mshauri wa matajiri waliotumia Benki ya Bear Stearns.
Mwaka 1981, alipoondoka Bear Stearns, Epstein alianzisha kampuni yake ya ushauri wa masuala ya kifedha na uhalifu wa kifedha, Intercontinental Assets Group Inc. (IAG). Ni kipindi hiki alipata utajiri wa haraka kwa njia nyingi za udanganyifu.
Kupitia IAG, Epstein aliweza kujenga ukaribu na matajiri pamoja na wanasiasa maarufu. Alijipambanua kama mshauri wa masuala ya kifedha wa Serikali ya Marekani, pamoja na matajiri. Aliinadi kampuni yake kuwa na uwezo wa kuokoa fedha zenye kuibiwa kitapeli.
Ana Obregón, nyota wa filamu, mzawa wa Madrid, Hispania, ni mmoja wa wateja matajiri wa Epstein. Mwaka 1982, Epstein alimsaidia baba yake Ana kuokoa mamilioni yake ya dola, kutokana na hati fungani zake kwenye taasisi ya Drysdale Securities. Taasisi hiyo ilifiliska mwaka 1982.
Mara, Epstein akawa anasafiri mara kwa mara kati ya Marekani, Ulaya na Mashariki ya Kati. Kipindi hiki. Epstein alijitambulisha kama ofisa wa shirika la ujasusi Marekani (CIA), inadaiwa pia kwamba mtaalamu huyo wa mambo ya fedha, alifanya kazi na Idara ya Intelijensia ya Uingereza. Na akawa anatumia hati ya kusafiria ya Australia.
Epstein, alishirikiana pia na mhalifu mwingine wa kimataifa, Steven Hoffenberg, aliyekuwa anaendesha mtandao wa kitapeli, unaoitwa Towers Financial Corporation (TFC). Uhusiano wake na matajiri, pamoja na wanasiasa wakubwa, ulimfanya Epstein kutoguswa na yeyote.
Mwishoni mwa miaka ya 1980, Epstein alianzisha kampuni aliyoiita J. Epstein & Company, ambayo alisema ni kwa ajili ya kusimamia mali za wateja wenye utajiri unaozidi thamani ya dola bilioni moja. Mwaka 1996, Epstein alibadili jina la kampuni yake na kuiita Financial Trust Company (FTC).
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, ambalo hujikita zaidi kwenye biashara, uwekezaji, ujasiriamali, uongozi na teknolojia, kati ya mwaka 1999 na 2008, FTC na kampuni nyingine ya Epstein, inayoitwa Southern Trust Company (STC), ziliingiza mapato ya dola milioni 800, nyingi zikitokana na kazi za mabilionea wawili, Leslie Wexner na Leon Black.
Kisiwa cha Mtakatifu Thomas, ndani ya Visiwa vya Virgin, kina mengi kuhusu Epstein. Alikitumia kukwepa kodi, kisha alianzisha makazi ambayo alikuwa akifanya hafla mbalimbali na kuwaalika watu maarufu, wengi wao ni matajiri wakubwa na wanasiasa.
Wasichana wadogo walisafirishwa hadi kisiwani na kutumikishwa kingono na Epstein mwenyewe, vilevile wageni wake walikirimiwa masaji ya ngono. Na kila kilichofanyika kisiwani humo, kilirekodiwa.
Hata kasri lake la Palm Beach, Florida, nalo alilitumia kufanya hafla zenye nakshi za ngono na watoto wadogo wa kike, akifurahi na wageni wake. Epstein pia angeweza kucheza kingono na watoto wa kike mbele ya wageni wake.
Inadaiwa kuwa matajiri na wanasiasa waliokubali ‘ofa’ za Epstein, za kustarehe na watoto wa kike, walirekodiwa kwa video na picha mnato bila wao kujua. Makasri ya Epstein yalitegwa kamera za siri, kuhakikisha kila chenye kufanyika ndani kinarekodiwa.
Polisi walipopekua nyumba ya Palm Beach mwaka 2006, walibaini kamera mbili za siri. Kasri lingine la Epstein, lililopo New York, nalo lilibainika kuwa na kamera nyingi. Nadharia ni kuwa watu wengi mashuhuri walirekodiwa na Epstein katika matukio machafu na watoto wa kike.
Video na picha mnato alizorekodi Epstein, inadaiwa alizitumia kuwatisha wateja wake, mosi wakamfanya kuwa tajiri zaidi, pili, kwa wanasiasa ili kupata ulinzi wa vitendo vyake vya kihalifu.
Kufanikisha kila kitu, kuanzia kutafuta watoto wa kike wa kuwatumikisha kingono mpaka kurekodi wateja wa matukio ya uhalifu, Epstein alishirikiana na mpenzi wake, Ghislaine Maxwell, ambaye ni raia wa UK.
Kwa sasa Ghislaine anatumikia kifungo cha miaka 20 kwenye Gereza la Bryan, Texas, baada ya kukutwa na hatia ya usafirishaji wa watu na kutumikisha watoto kingono.
Shinikizo kuhusu Mafaili ya Epstein linatokana na majina makubwa ambayo inaaminika yamo, akiwemo Trump, ambaye alipata kuwa rafiki wa Epstein. Ikumbukwe, Epstein alifariki dunia kipindi Trump alipokuwa madarakani katika muhula wake wa kwanza.
Watu wa karibu na Epstein, wamekuwa wakikumbwa na kashfa pamoja na mashitaka. Bilionea Leon Black, mwaka 2021, alifikishwa mahakamani kwa kesi ya ubakaji.
Mlalamikaji, Cheri Pierson, alisema Black alimbaka mwaka 2002 kwenye kasri la Epstein, New York.
Kesi nyingine dhidi ya Black ilifunguliwa Julai 25, 2025, ikidaiwa bilionea huyo alimbaka binti wa miaka 16 mwenye utindio wa ubongo mwaka 2002, ndani ya jumba la Epstein, Manhattan.
Februari 19, 2022, mshirika wa Epstein, Jean-Luc Didier Henri Brunel, alikutwa amejiua kwenye Gereza la La Sante, Paris, Ufaransa, alipokamatwa na kushikiliwa kwa makosa ya ubakaji. Brunel alikuwa gwiji wa mitindo, alianza kujificha baada ya Epstein kujiua, kabla ya kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle, Paris, akijaribu kutorokea Dakar, Senegal.
Novemba 19, 2025, Bunge la Marekani, chemba zote mbili (Congress), lilipitisha sheria inayoitwa Epstein Files Transparency Act, ambayo ilimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka hadharani nyaraka zote kwenye Mafaili ya Epstein, ndani ya siku 30, tangu kusainiwa kwa sheria hiyo.
Congress waliamua kulivalia njuga suala hilo baada ya kuona uongozi wa Trump ulikuwa ukipiga danadana.
Januari 30, 2026, kurasa milioni tatu, picha 180,000, video 2,000 na barua pepe, viliachiwa. Ndani ya mafaili hayo, Trump yumo ndani, vilevile mabilionea Elon Musk, Bill Gates, Richard Branson, mwanamfalme, Andrew Mountbatten-Windsor, na mwanamkakati wa zamani wa Trump, Steve Bannon.
Waziri wa Fedha wa zamani wa Marekani, Larry Summers, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak, Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ni miongoni mwa majina ndani ya Mafaili ya Epstein. Bado kurasa milioni 3.5 hazijaachwa wazi.
Hofu kwa Trump na wengine wote, ni je, watatajwa kuhusika na vitendo vya uhalifu wa kingono dhidi ya watoto? Vyovyote iwavyo, hivi sasa Trump na wenzake, kila wanaposikia habari za Mafaili ya Epstein, inakuwa mithili ya simulizi za jehanamu.