Huko Prisons kimenuka, Otieno anahesabiwa saa tu

‘LOLOTE linaweza kutokea’. Ni kauli ya Mtendaji Mkuu wa Tanzania Prisons, Godfrey Madegwa akielezea hatma ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya Zedekiah Otieno kutokana na matokeo yasiyoridhisha iliyonayo maafande hao wa Magereza.

Habari za ndani zilizonaswa na Mwanaspoti zimedai Otieno alipewa mechi tatu ikiwa ni kipimo cha mwenendo alionao klabuni, ambapo mechi ya jana dhidi ya Coastal Union ndio ilikuwa ya mwisho kuamua hatma yake kikosini.

Katika mechi hiyo, TZ Prisons ikiwa uwanja wa nyumbani wa Sokoine, jijini Mbeya na kujikuta ikichakazwa kwa mabao 4-1 huku ikionesha kiwango duni na kufanya presha kuwa kubwa zaidi ndani na nje ya uwanja.

Tangu kutua kikosini, Otieno ameiongoza timu hiyo michezo 12 akishinda miwili, sare tatu na kupoteza saba na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Madegwa amesema licha ya kwamba hawajafikia muafaka na kwamba wanaendelea kujadiliana pande zote na kitakachofikiwa wataweka wazi juu ya hatma ya kocha huyo.

Amesema kwa sasa wanapitia wakati mgumu wa kupata matokeo na kukiri kuwa presha imekuwa kubwa nje na ndani ya uwanja akibainisha kuwa wanaendelea kuwajenga wachezaji kiakili na kisaikolojia ili kutokata tamaa.

“Lolote linaweza kutokea, taarifa ni kweli zipo na makao makuu wataeleza zaidi, kazi ya kocha ni kufundisha na akikosa matokeo lazima atupe maelezo, akishindwa kujieleza na kutoa majibu sahihi hakuna haja ya kuendelea naye,” amesema Mtendaji Mkuu huyo wa TZ Prisons aliyeongeza;

“Bado tuko naye ukizingatia mifumo ya timu yetu mambo yote yanatoka makao makuu, hii ni taasisi hatuwezi kufanya uamuzi kwa mihemko, lazima tukubaliane pande zote na kitakachoazimiwa tutaweka wazi.”

Kigogo huyo ameongeza, uongozi unaendelea kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo kwa kutuliza presha kwa wachezaji ili mechi zilizobaki wanafanya vizuri na kuondokana na mzimu wa kila msimu kusubiri huruma dakika za mwisho.