BALOZI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA NEEMA LUGANGIRA, ADDIS ABABA ETHIOPIA

*********

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Women Political Leaders (WPL), Neema Lugangira, kuhusu ushirikiano wa kikazi katika kuwaendeleza wanawake.

Akizungumza jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo, Balozi Mulamula alisema amefurahi kukutana na kiongozi huyo ofisini kwake nakujadiliana naye masuala mbalimbali ya kuwaendeleza wanawake.

“Nimefurahi kukutana na Mh.Neema Lugangira ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Women Political Leaders (WPL), nimempongeza kwa nafasi hiyo na kumuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake. Kiongozi huyu namfahamu nilikuwa naye bungeni Tanzania, ni mchapakazi na, mpenda maendeleo naamini atakuwa msaada mkubwa kwa wanawake,” alisema.

Alisema katika mazungumzo yao, wamejadiliana kuimarisha ushirikiano wa wanawake katika siasa, hususan katika muunganiko wa amani, usalama na misaada ya kibinadamu; na wamekubaliana kushirikiana kupitia ofisi zao.

Kwa upande wake, Katibu wa WPL, Neema Lugangira, alimpongeza Balozi Mulamula kwa kwa kuteuliwa kuwatumikia wanawake wa Afrika na utumishi uliotukuka anaoendelea nao huku akimuahidi ushirikiano katika utekelezaji majukumu yake.

0000