Dodoma. Taasisi ya Aga Khan kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kupitia mradi wa Tuinuke Pamoja imepanga kutumia Sh7 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu kuchangia katika harakati za kufikia usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke kwa kuviwezesha vikundi vya kijamii kwenye halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma.
Vikundi hivyo kutoka halmashauri za Wilaya ya Kondoa Vijijini, Kondoa Mji, Bahi, Chamwino, Dodoma Mjini na Chemba, wanufaika wakubwa katika mradi huo ni wanawake, watu wenye ulemavu na vijana.
Wakizungumza jana Jumatatu, Februari 2, 2026 kwenye uzinduzi wa Mradi wa Tuinuke Pamoja uliofanyika wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, wanufaika wa mradi huo wamesema maisha yao yamebadilika baada ya kufadhiliwa na Aga Khan Foundation.
Mweka Hazina wa Kikundi cha wanawake Tujikomboe Makamaka kutoka wilayani Chemba, Veronica Banari amesema kupitia ufadhili wa Aga Khan Foundation wamefanikiwa kuanzisha kilimo cha bustani za mboga mboga na kununua vyerehani kwa ajili ya shule ya ushonaji.
Amesema mpaka sasa wana wanafunzi watano ambao wamejiunga kwa ajili ya mafunzo ya kushona nguo mbalimbali. Mafunzo ambayo yanatolewa bure kwa wasichana na wanawake ambao wanakabiriwa na changamoto za kifedha kujiendeleza. Kikundi kimejidhatiti kuhakikisha sehemu ya wanawake na wasichana wenye uhitaji wanapata taaluma kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi, kujitegemea na kupunguza utegemezi.
Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan (mwenye shati la rangi ya kijani) akiwa amepanda kwenye pikipiki inayotumia umeme ambayo imetolewa kwa wahudumu wa Afya kwa ajili ya kuhudumia jamii Wilayani Chamwino, Chemba na Mpwapwa, katika hatua inayofuata ni kufikia halmashauri za Kondoa na Kongwa. Picha na Rachel Chibwete”
“Aga Khan Foundation Tanzania imetuwezesha Sh27.5 milioni ambazo zimetusaidia kuanzisha miradi mbalimbali ikiwamo ufugaji wa kuku wa kisasa na tuna mpango wa kujenga banda kubwa la kisasa lenye uwezo wa kuhifadhi kuku 2,000 kutoka 450 tulionao sasa, lakini kupitia fedha hizo tumefanikiwa kutengeneza pedi za kike ambazo tunazigawa kwa wanafunzi walioko shuleni ili kuwahakikisha hedhi salama na hakuna msichana anaekosa masomo kwasababu ya hedhi,” amesema Balie.
Amesema awali kabla ya ufadhili walikuwa wanafanya miradi mbalimbali lakini hawakuona faida yake, baada ya ufadhili wameanza kupata faida inayowawezesha kuboresha maisha yao, hususani baada ya kupatiwa mafunzo ya kina kutoka Tuinuke Pamoja kuhusu usimamizi wa miradi yetu, utunzaji wa fedha na uwekaji wa kumbukumbu.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Amkeni Wanawake Viziwi kutoka Wilaya ya Bahi, Helena Banjilwa amesema kikundi hicho kinaundwa na wanawake watatu viziwi walioamua kujikita kwenye uzalishaji wa siagi ya karanga.
Amesema waliamua kujiunga kwenye kikundi kwa kuwa walikuwa wanapitia changamoto nyingi kutokana na ulemavu walionao ikiwamo unyanyapaa, hivyo ili kujikwamua walijiunga na kuweka nguvu zao pamoja katika kikundi ili watumie fursa zilizopo ikiwamo ufadhili wa Aga Khan Foundation Tanzania.
Amesema kupitia ufadhili huo, wamepewa elimu ya ujasiriamali, kujua fursa za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo zilizopo kwenye maeneo yao ikiwamo haki za binadamu na haki za watu wenye ulemavu na usawa wa kijinsia.
“Aga Khan Foundation imetuwezesha kusimama sisi wenyewe na sasa tunajiamini,” amesema Banjilwa.
Meneja Mradi kutoka Aga Khan Foundation, Nestory Mhando amesema jumla ya vikundi 21 kutoka halmashauri tatu za Mkoa wa Dodoma (Kondoa Mji, Kondoa Vijijini, na Chemba) vimenufaika kwa kujengewa uwezo na kupatiwa ruzuku kwa ajiri ya utekelezaji wa miradi yao, na vikundi 36 kutoka Bahi, Dodoma Jiji na Chamwino viko katika hatua ya kujengewa uwezo kabla ya ufadhili, na Halmashauri za Kongwa na Mpwapwa zitaingia katika hatua inayofuata ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa Sh7 bilioni kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Amesema wanufaika wa mradi huo ni vikundi vya kijamii vilivyoko ngazi ya vijiji, kata na vitongoji vilivyoundwa na wanawake pamoja na vikundi vya watu wenye ulemavu na vijana vilivyosajiliwa kwenye ngazi ya halmashauri, lengo likiwa ni kuwainua ili waweze kujitegemea kiuchumi na kuchangia katika kufikia usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Aga Khan Foundation, Atteeya Sumar amesema kwa kipindi cha nusu ya utekelezaji wa mradi huo wameona matokeo chanya kwa vikundi walivyovidhamini.
Amesema vikundi vimepewa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali, utunzaji wa fedha, elimu ya biashara, utunzaji wa mazingira na kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii yao ikiwamo ukeketaji.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu (kushoto), akizungumza na wanawake wa Kikundi cha Tujikomboe Makamaka kutoka Wilayani Chemba kwenye uzinduzi wa mradi wa Tuinuke Pamoja uliofanyika Wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema nusu ya kwanza ya kipindi cha mradi huo wamewafikia jumla ya wanufaika 10,969 wakiwamo wanawake 6,224 na wanaume 4,745 kwenye halmashauri za Kondoa mjia, Kondoa Vijijini na Chemba.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Tuinuke Pamoja, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Felister Mdemu amewataka wanufaika wa mradi huo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuimarisha uchumi wao.
Amesema Aga Khan Foundation Tanzania imewaamini na kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha, hivyo wasimwangushe.