BAADA ya ushindi dhidi ya Mashujaa ikifikisha pointi 27 kwenye mechi 15 ilizocheza, JKT Tanzania imebakiza tatu za ushindi ambazo ni sawa na pointi tisa ili kufikia rekodi ya alama 36 ilizokusanya msimu uliopita katika mechi zote za msimu.
Ipo hivi, msimu uliopita baada ya mechi 15 JKT Tanzania ilikuwa imekusanya pointi 19 wakati huu hadi sasa ina alama 27 ikiwa inaongoza msimamo na maana yake ni kwamba imeongeza nane zaidi.
Msimu huu JKT Tanzania imeshinda mechi sita wakati uliopita ilishinda nne, imepoteza mbili dhidi ya Simba na Dodoma Jiji ikiwa ni mbili pungufu ya msimu uliopita baada ya 15 na sare ni mechi sita sita, moja pungufu ya uliopita.
Msimu uliopita baada ya mechi 15 ilifunga mabao manane na kuruhusu tisa wakati huu imefunga 19 na kuruhusu tisa.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema siri ya ubora na mafanikio wanayoyapata ni kuzingatia kufanya maboresho kwenye mechi za nyuma na kuendelea kuwa bora zaidi. “Licha ya kutokuwa na wakati mzuri kutokana na ratiba tumekuwa tukizingatia kufanyia kazi upungufu wetu wa mechi za nyuma. Ligi ni ngumu na wapinzani ni bora. Mipango na mikakati imara ndio inatupa matokeo mazuri,” amesema.
“Kukubali kupokea upungufu uwanja wa mazoezi kwa wachezaji wangu ndio siri ya ubora ambao tunao msimu huu. Tunapambana kuhakikisha hatupotezi (mechi) kizembe, tukiwa na nafasi ya kushinda zaidi ni kuangalia namna ya kutumia nafasi.”
Ahmed amesema anafurahia kuvunja rekodi nyingi za msimu uliopita kuanzia pointi, mabao na kuongeza mechi za kushinda huku wakiwa katika nafasi bora na wanaamini kuna rekodi nzuri wataiandika msimu huu.