Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imekubaliana na hoja moja ya pingamizi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kuhusiana kizimba cha mashahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili, kuwa kizimba hicho hakistahili kutumika.
Lissu aliweka pingamizi akipinga shahidi wa nne wa Jamhuri katika kesi hiyo ambaye ni miongoni mwa mashahidi 11 wa Jamhuri waliopewa ulinzi wa mahakama kwa maana ya kutoa ushahidi wao bila kuonekana, akidai kuwa kizimba hicho hakiendani na matakwa ya kanuni ya 3 ya Kanuni za Ulinzi wa mashahidi, kwani hakiiwezeshi mahakama kumuona shahidi huyo.
Mahakama katika uamuzi wale leo Jumatano, Februari 11,2026 uliotolewa na kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Dunstan Ndunguru amekubaliana na hoja ya Lissu kuwa kizimba hicho hakikidhi matakwa ya kanuni hiyo kwani mahakama haiwezi kumuona shahidi huyo akiwa kizimbani humo.
Hivyo mahakama imeelekeza kizimba hicho kirekebishwe kwa namna ambayo mahakama itaweza kumuona shahidi husika na imeahirisha kesi hizo mpaka kesho kupisha marekebisho ya kizimba hicho.
Mbali na hoja hiyo moja mahakama imekataa hoja nyingine nne za Lissu za pingamizi hilo ikiwa ni pamoja na uhalali wa mashahidi hao fiche wa Jamhuri.
Endelea kufuatilia Mwananchi