Dar es Salaam. Leo, Februari 11, Tanzania inaungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, maadhimisho yanayolenga kutambua mchango wao katika maendeleo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), huku yakihamasisha kizazi kipya cha wasichana kuthubutu kuingia katika taaluma hizo.
Hapa nchini, maadhimisho haya kitaifa yanafanyika jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu: ‘Muunganiko wa Akili Unde Sayansi ya Jamii, STEM na Fedha kuelekea Dira 2050: Kujenga Mustakabali Jumuishi kwa Wanawake na Wasichana’.
Maadhimisho haya yanafanyika wakati mjadala wa usawa wa kijinsia katika elimu ya sayansi ukiendelea kushika kasi, huku takwimu zikionyesha bado kuna pengo kati ya wavulana na wasichana katika masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya sekondari hadi vyuo vikuu.
Wadau wa elimu wanasema changamoto hizo ni pamoja na mitazamo hasi ya kijamii, ukosefu wa mifano ya kuigwa, rasilimali haba shuleni na mazingira yasiyowezesha wasichana kujikita katika masomo ya sayansi.
Akizungumza na Mwananchi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mwanaidi Mlay amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali, bado kunahitajika msukumo wa makusudi kubadili fikra potofu kwamba sayansi ni taaluma za wanaume.
“Wasichana wana uwezo sawa na wavulana. Tatizo si akili, bali ni mazingira na imani tulizojijengea kama jamii. Tukibadilisha mtazamo, tutaona mabadiliko makubwa,” amesema.
Katika shule nyingi za sekondari, hususan maeneo ya vijijini, uhaba wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi umeendelea kuwa kikwazo kikubwa.
Mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Aisha Salum, anasema alipata hamasa ya kusoma mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia) baada ya kushiriki katika kambi ya sayansi iliyoandaliwa na taasisi binafsi.
“Nilipowaona wanawake wahandisi na madaktari wakizungumza nasi, nilijiona na mimi naweza. Kabla ya hapo nilikuwa naogopa fizikia, hasa nilipokuwa nasikia masomo ya sayansi ni magumu,” amesema.
Hata hivyo, safari ya wasichana katika sayansi si nyepesi. Baadhi yao hukumbana na changamoto za kifamilia na kijamii, ikiwamo shinikizo la kuolewa mapema au kuhamasishwa kuchagua kozi zinazoonekana rahisi au zinazofaa zaidi kwa wanawake.
Mwanasaikolojia wa elimu, Stela Mbise amesema malezi yana mchango mkubwa katika kuwajengea wasichana kujiamini.
“Mzazi ukimwambia mtoto wa kike tangu akiwa mdogo kwamba anaweza kuwa mwanasayansi, unamjengea msingi imara wa kuamini katika uwezo wake,” amesema.
Kwa upande wa Serikali, kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuimarisha elimu ya sayansi, ikiwamo ujenzi wa maabara, utoaji wa mafunzo kwa walimu na kuhamasisha wanafunzi kuchagua masomo ya sayansi.
Pia, vyuo vikuu na taasisi za utafiti zimeanza kuweka programu maalumu za kuwalea na kuwashauri wasichana wanaosomea taaluma za STEM ili wasikate tamaa njiani.
Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na kuhamasisha wasichana katika teknolojia, Girls in Tech, Neema Joseph, amesema mapinduzi ya kidijitali yamefungua milango mipya kwa wanawake.
Amesema maendeleo ya sayansi hayawezi kuwa kamili bila sauti, akili na ubunifu wa wanawake na wasichana. Hivyo, ametaka siku hii iwe mwendelezo wa hatua madhubuti za kuhakikisha usawa si kauli mbiu tu, bali ni uhalisia unaoonekana katika maabara, vyuoni na kwenye taasisi za utafiti kote nchini.
“Leo hii, msichana anaweza kujifunza programu za kompyuta akiwa nyumbani kupitia mtandao. Tunachohitaji ni kuhakikisha wanapata vifaa na intaneti, hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Wakati dunia ikiadhimisha siku hii, ujumbe mkubwa unabaki kuwa mmoja: kumpa msichana nafasi ya kusoma sayansi si hisani, bali ni haki yake ya msingi. Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha ndoto za wasichana hazizimwi na mila potofu, umaskini au kukosa fursa,” amesema.
Licha ya changamoto, zipo hadithi nyingi za mafanikio zinazotoa matumaini. Kuna wanawake Watanzania wanaofanya vizuri katika utafiti wa afya, nishati jadidifu, kilimo cha kisasa na teknolojia ya habari.
Wapo wanaoongoza miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa, wakionyesha wazi kuwa jinsia si kigezo cha uwezo wa kitaaluma.
Wadau wanasema ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika sayansi, kunahitajika mkakati wa pamoja unaohusisha Serikali, sekta binafsi, shule na familia.
Miongoni mwa mapendekezo ni kuanzisha na kuziendeleza klabu za sayansi shuleni, kutoa ufadhili maalumu kwa wasichana wa sayansi, pamoja na kuandaa mashindano ya ubunifu yatakayowapa jukwaa la kuonyesha vipaji vyao.
Wataalamu wanasema bila kuwashirikisha wanawake kikamilifu katika utafiti na ubunifu wa kisayansi, dunia itakuwa inajinyima nusu ya uwezo wake wa kutatua matatizo.
Kwa Tanzania, ambako uchumi wa viwanda na teknolojia unazidi kupewa kipaumbele, kuwekeza kwa wasichana katika sayansi ni sawa na kuwekeza katika mustakabali wa taifa.
“Tukitaka kuwa na viwanda vyenye ushindani, hospitali zenye wataalamu wa kutosha na sekta ya Tehama yenye ubunifu, lazima tuanze leo kuwaandaa wasichana wetu.
“Kwa wasichana wanaoota kuwa madaktari, wahandisi, watafiti au wabunifu wa teknolojia, siku ya leo iwe chachu ya kujiamini na kusonga mbele. Na kwa jamii, iwe ni kengele ya kuamka na kuondoa vikwazo vyote vinavyowazuia kung’ara katika anga la sayansi,” amesema Dk Mlay.