Mwanza. Serikali mkoani Mwanza imezitaka halmashauri za mkoa huo kufanya tathmini ya kina kubaini changamoto na upungufu wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari, badala ya kusubiri ziibuliwe kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza Februari 10, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Masemele iliyopo Wilaya ya Ilemela, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kubaini na kuibua changamoto katika sekta ya elimu na kuziainisha mapema kutarahisisha kupatiwa fedha za utekelezaji na kukabiliana na changamoto hizo.
Mtanda amesema si busara kwa changamoto za shule kusubiri kuibuliwa kwanza kupitia mitandao ya kijamii ndipo hatua zichukuliwe, badala yake tathmini ifanyike mapema ili kuzuia aibu na usumbufu kwa wanafunzi.
“Ni aibu kubwa kuona wanafunzi wamekaa chini, halafu picha zinasambazwa mitandaoni ndipo tuanze kukimbizana kutafuta suluhu. Tusifike huko,” amesema Mtanda.
Ameeleza amekuwa akipokea ujumbe kutoka kwa wazazi wakilalamikia uhaba wa madawati katika baadhi ya shule za wilaya hiyo na kutaka tathmini ifanyike kwa shule zote za msingi na sekondari ili kubaini maeneo yenye upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na miundombinu mingine muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akitoa maelekezo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Masemele iliyopo Wilaya ya Ilemela.
“Ili fedha zitakapopatikana zielekezwe moja kwa moja kwenye mahitaji hayo,”amesema Mtanda.
Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya elimu kuelewa mazingira yao na kuweka vipaumbele kulingana na uhitaji mkubwa uliopo katika maeneo yao.
Kuhusu ujenzi wa maabara shuleni hapo, Mtanda ametoa maagizo ya kukamilika kwa ujenzi wa maabara hiyo ndani ya wiki mbili, pamoja na kukamilisha uwekaji wa nishati ya umeme katika chumba kimoja cha maabara na kuweka tenki la maji ili kuwezesha matumizi bora ya miundombinu hiyo.
Katika hatua nyingine, Mtanda amewataka wakazi mkoani Mwanza kuchangamkia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia huduma bora za afya wakati wote, hasa wanapougua ghafla na hawana pesa za matibabu.
Akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kayenze, Mtanda amesema mahitaji muhimu kwa binadamu ni chakula, afya na makazi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anajilinda kiafya kwa kukata bima ya afya kwa ajili ya ustawi wa maisha yake na familia yake, ambapo kila kaya itachangia Sh150,000 kupata huduma hiyo kwa watu sita.
Tayari baadhi ya wakazi wa jijini Mwanza waliojiunga na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wamepata kadi za bima hiyo na kuishukuru Serikali kwa kujali afya za Watanzania hasa wenye kipato cha chini.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (wa tatu kushoto) akikagua ujenzi wa zahanati ya Nyambiti iliyopo wilayani Ilemela.
“Nimepata kadi zangu sita… tano ni za watoto wangu, moja ni ya kwangu. Ningeiomba Serikali iangalie namna ya kutusaidia sisi wenye watoto zaidi ya watano maana mtoto wangu mmoja amekosa kadi ya bima kwa kuwa idadi ya watu wanaopewa ni sita tu, lakini mimi nina watoto sita hivyo mmoja hajapata,” amesema Kulwa Kwandu, mkazi wa jijini Mwanza.
Mtanda anafanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika sekta za elimu na afya mkoani Mwanza ambapo mpaka sasa tayari amekagua miradi hiyo katika kata za Wilaya ya Ukerewe na Ilemela.