Equity kukusanya Sh200 bilioni kusaidia biashara ndogo

Dar es Salaam. Benki ya Equity imelenga kukusanya Sh200 bilioni kupitia uwekezaji wa wateja ili kuongeza uwezo wa ufadhili na kukuza utoaji wa mikopo, hususan kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs).

Hatua hiyo itatekelezwa kupitia akaunti maalumu ya amana ya muda wa miaka mitatu iitwayo ‘Wekeza’, inayoruhusu uwekezaji kuanzia Sh500,000 na kutoa faida ya asilimia 13 kwa mwaka, itakayolipwa kila mwezi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa akaunti hiyo leo Jumatano, Februari 11, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo, wa Kati, Wakubwa na Binafsi wa benki hiyo, Theresia Mayanie, amesema lengo ni kuwahamasisha Watanzania kuanza kuwekeza sasa kwa ajili ya kesho yao.

“Akaunti hii inalenga kukuza na kulinda mitaji ya watu binafsi, wajasiriamali na taasisi kupitia uwekezaji salama unaotoa faida ya asilimia 13 kwa mwaka,” amesema.

Ameeleza kuwa mteja ataweza pia kutumia amana yake kama dhamana ya hadi asilimia 80 ya thamani ya uwekezaji huo ili kupata mkopo bila kuvunja akaunti yake.

Dirisha la kuwekeza limefunguliwa rasmi Februari 11, 2026 na litafungwa Aprili 30, 2026.

“Tutalipa faida kila mwezi, na baada ya miaka mitatu mteja atarejeshewa mtaji wake iwapo atahitaji,” amesema Mayanie, akiongeza kuwa mpango huo unalenga kuongeza uhuru wa kifedha kwa Watanzania na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Equity Bank, Shumbana Walwa, amesema benki hiyo imeanzisha akaunti hiyo ili kuwapa wateja wake fursa ya kukua kifedha sambamba na huduma za kibenki wanazopata.

“Tunataka kuhakikisha ndoto za wateja wetu zinawezeshwa kuanzia sasa, siyo tu kupitia miamala bali pia uwekezaji wenye tija,” amesema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, George Fumbuka, ameipongeza Equity kwa ubunifu huo, akisema ni njia mojawapo itakayowasaidia Watanzania kupata mapato ya ziada kupitia uwekezaji salama.