Malisa aomba tena ahirisho, kesi yake yakwama kuendelea

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imeahirisha usikilizaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai ya makosa ya kimtandao inayomkabili Mchungaji Godfrey Malisa, baada ya mshtakiwa huyo kuomba ahirisho akisubiri msaada wa kisheria kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Februari 11, 2026, mahakama hiyo ilipanga kuanza kusikiliza mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri. Hata hivyo, Malisa aliomba ahirisho akieleza kuwa hana wakili kwa sasa na anasubiri majibu kutoka TLS makao makuu kuhusu kupewa uwakilishi wa kisheria.

Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama, anayesikiliza shauri hilo, alimweleza mshtakiwa kuwa hilo ni ahirisho la mwisho na kwamba kesi hiyo lazima ianze kusikilizwa Februari 12, 2026. Alifafanua kuwa mahakama iliahirisha mashauri mengine matano ya madai ili kupisha usikilizaji wa kesi hiyo, akisisitiza kuwa mashauri ya aina hiyo ni matatu katika eneo hilo.

“Kesi zikifika mahakamani zinatakiwa zisikilizwe kama mahakama ina mamlaka ya kuisikiliza. Kesi za aina hii ziko tatu; jana imesikilizwa moja na mashahidi wawili wametoa ushahidi. Mimi ndiye Mfawidhi wa Mahakama za mkoa, najua kinachoendelea. Hii peke yake ndiyo haijaanza kusikilizwa,” amesema Hakimu Mkama.

Ameongeza kuwa kuanzia sasa mshtakiwa aendelee kufuatilia TLS, lakini kesho saa tatu asubuhi afike mahakamani kwa ajili ya kuanza usikilizaji, akiamini hakutakuwa na sababu nyingine ya kuahirisha.

Ilielezwa mahakamani kuwa maombi ya Malisa kupewa msaada wa kisheria yaliwasilishwa Februari 10, 2026, na TLS Moshi wamewasiliana na makao makuu kusubiri idhini ya kumpatia wakili. Mbali na kesi hiyo ya kimtandao, Malisa pia anakabiliwa na kesi nyingine ya uhaini.

Februari 4, 2026, kesi hiyo iliahirishwa baada ya Malisa kueleza kuwa amepewa nyaraka za mashahidi na vielelezo siku hiyo asubuhi, hivyo kuhitaji muda wa kuzipitia pamoja na wakili wake. Upande wa Jamhuri ulithibitisha kumpatia nyaraka hizo na kuiachia mahakama iamue kuhusu ombi la kuahirisha.

Katika kesi ya jinai namba 28411/2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa katika akaunti yake ya YouTube iitwayo “Godfrey Malisa”, akidai kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu kwa madai ya kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania. Maneno hayo yanadaiwa kuchapishwa Novemba 15, 2025, katika eneo la Miembeni, wilayani Moshi.

Hati ya mashtaka iliyofunguliwa Novemba 3, 2025, inanukuu kauli inayodaiwa kuchapishwa: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.” Upande wa Jamhuri unadai Malisa alichapisha taarifa hizo akijua hazikuwa sahihi na kwa lengo la kupotosha umma.

Katika kosa la pili, anatuhumiwa kwa uchochezi kinyume cha kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023. Inadaiwa kuwa siku hiyohiyo alichochea umma kufanya mkusanyiko usio halali, kinyume cha sheria.

Mbali na mashtaka hayo, Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali nchini.

Kwa upande wa historia yake ya kisiasa, Malisa aliingia kwenye siasa mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia TLP. Mwaka 2015 aligombea urais kupitia CCK na baadaye uspika. Mwaka 2018 aligombea ubunge Kinondoni kupitia TLP, na mwaka 2020 aligombea ubunge Moshi Mjini kwa tiketi ya NCCR Mageuzi.

Baada ya uchaguzi wa 2020 alijiunga na CCM, lakini Februari 10, 2025 alifukuzwa uanachama. Uamuzi huo ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, kwa maelezo kuwa Malisa alikosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kutokana na kupinga maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.

Pamoja na kufukuzwa, Malisa aliendelea kupinga uteuzi huo kupitia mahakamani na mitandao ya kijamii.