Mgunda alia na Yona Amos

KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema kipigo cha bao 1-0 ilichopewa timu hiyo ugenini na Pamba Jiji kimewashtua, kwani hawakutarajia huku akimtaja kipa Yona Amos aliyechangia kuziacha pointi tatu jijini Mwanza.

Namungo ilipata kipigo hicho cha tatu msimu huu katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuiacha isalie nafasi ya tano ikiwa na pointi 20 baada ya mechi 13, huku Pamba ikienda hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 23 kupitia mechi 14.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema Namungo imefungwa kwa umahiri na ubora wa Amos ambaye licha ya kuokoa michomo ya mastaa wa Wauaji wa Kusini, lakini kitendo cha kudaka penalti ya Fabrice Ngoy kiliwaua kabisa.

Namungo iliyokuwa ikikamilisha mechi tatu mfululizo ugenini imeambulia pointi mbili ikianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate, pia ilipata pointi moja dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya sare ya 1-1 kabla ya kipigo cha Pamba Jiji.

Mgunda alisema ameyapokea matokeo licha ya kutokuwa katika malengo kwani walitamani kupata walau pointi moja na si kupoteza wakiwa ugenini huku akimtaja Amos kuwa kikwazo. “Mchezo ulikuwa mzuri kwa pande zote mbili. Mbinu zetu bora kwa mabenchi yote mawili zilitoa mechi nzuri ya ushindani kosa moja walilolifanya Pamba Jiji tukipata penalti tulishindwa kulitumia vyema kutokana na ubora wa mlinda mlango,” alisema.

“Kipindi cha pili wapinzani walirudi kwa kasi na kutuadhibu. Haikuwa rahisi, lakini walifanikiwa kubaki na pointi tatu nyumbani. Walikuwa bora, nimekubali matokeo narudi na timu uwanja wa mazoezi kusawazisha makosa na kuendelea na mechi nyingine zilizo mbele yetu.”

Kocha huyo alisema pointi mbili walizopata ugenini kati ya mechi tatu walizocheza zina faida kwani anaamini zimekuwa sehemu ya ushindi na wataendelea kupambana kuhakikisha uwanja wa nyumbani hawafanyi kosa.

Kwa upande wake, Amos akizungumzia penalti aliyoidaka na kuizuia Namungo kupata angalau pointi moja haikuwa rahisi kwake kuibeba Pamba uwanja wa nyumbani baada ya kuibuka.

Amos alisema siri kubwa ya kudaka penalti ya Ngoy aliyekuwa anasaka bao la saba Ligi Kuu msimu huu ilitokana na kujiamini na kuweka presha pembeni wakati inapigwa.

“Kuhusu ile penalti nilimsoma vizuri mpigaji kabla ya kupiga na kuwa na wakati mzuri langoni bila presha hiki ndio kitu kilinipa imani kuwa naweza kudaka na ndicho kilichotokea baada ya tukio kufanyika,” alisema kipa huyo.

“Kuokoa mkwaju wa penalti ni kujiamini na kutokuwa na uoga wowote uwapo katika milingoti mitatu ua goli aliyekosa ni mpigaji mzuri amekutana na mimi nikiwa katika hali nzuri ya kuipambania timu.”

Amos alisema kama sio ujasiri alioufanya Pamba Jiji ilikuwa ikienda kupoteza katika dakika za jioni kipindi cha kwanza na wachezaji wenzake walirudisha morali ya ushindani na kusikiliza vizuri maelekezo ya benchi la ufundi kitu kilichowapa matokeo mazuri nyumbani. “Mpira ni mipango baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kushindwa kupata matokeo kocha alitoa maelekezo ambayo sisi kama wachezaji tuliyafanyia kazi na ndio yaliyotupa matokeo mazuri,” alisema Amos.

“Ushirikiano mzuri baina ya benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla ndio siri ya ubora wa timu na mimi kuweza kuibuka kuwa mchezaji bora wa mchezo imeniongezea morali ya kupambana zaidi.”