Wagosi wamaliza gundu la siku 76

USHINDI wa mabao 4-1 ilioupata Coastal Union mbele ya Tanzania Prisons umeiwezesha kuondoa jinamizi la siku 76 bila ushindi Ligi Kuu Bara, huku kocha Mohammed Muya akisema haikuwa rahisi kwani bado wanaijenga timu.

Wagosi wa Kaya walipata ushindi mara ya mwisho miezi miwili na siku 15 walipoinyoa Mbeya City mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Novemba 26, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Kabla ya ushindi wa juzi ugenini dhidi ya TZ Prisons, walisota mechi sita wakipoteza tatu dhidi ya Yanga (1-0), Azam FC (3-0) na kufungwa 3-0 na Pamba Jiji, huku wakitoka suluhu na Mashujaa na sare ya 1-1 ka KMC na TRA United.

Akizungumza na Mwanaspoti, Muya alisema wamepitia wakati mgumu wakipambana kujenga timu ambayo haikuwa bora kuanzia mwanzo wa msimu hadi sasa wakiamini wana kazi ya kufanya kuibakisha Ligi kuu.

“Kidogo wachezaji wanaanza kuelewa mfumo hii ni kutokana na timu kuanza upya kwa kufanya usajili mkubwa dirisha dogo bado nina kazi ya kufanya kuhakikisha naiweka timu kwenye ushindani,” alisema Muya.

“Ni mwanzo mzuri kwetu naamini matokeo haya yataongeza morali kwa wachezaji wangu ambao wanaipambania nembo ya Coastal sio rahisi kuanza moja na kuwa bora hivyo naamini kwa hiki kilichofanyika ni sehemu ya matunda ya uvumilivu.”