12,000 waajiriwa kampuni za kigeni Zanzibar, vijana waitwa

Unguja. Zaidi ya wazawa 12,244 wameajiriwa na kampuni za kigeni zinazoendesha shughuli zake Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini bado ipo changamoto ya baadhi ya vijana kushindwa kujitokeza au kuchangamkia fursa zilizopo.

Hayo yameelezwa leo Februari 11, 2026, katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, alipokuwa akijibu hoja za wajumbe.

Amesema kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya wazawa 12,244 wameajiriwa katika miradi mbalimbali ambapo Unguja wameajiriwa 10,848 na Pemba 1,396. Kati ya hao, Unguja wanawake ni 3,970 na wanaume 6,878, huku Pemba wanawake wakiwa 446 na wanaume 950.

Shariff alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Wawi, Bakari Hamad Bakari, aliyetaka kujua namna Serikali inavyotathmini ajira kwa wazawa katika kampuni za nje, kufuatia malalamiko kuwa baadhi ya nafasi zinachukuliwa na wageni.

Waziri amesema licha ya juhudi za Serikali, bado kuna changamoto ya mtazamo kwa baadhi ya vijana.

“Fursa zipo, lakini wakati mwingine vijana hawazichangamkii. Hivyo mwekezaji analazimika kutafuta watu wengine kujaza nafasi,” amesema.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiendelea na mkutano wa pili Baraza la 11 Chukwani Unguja Zanzibar



Ameeleza kuwa wizara kupitia Kamisheni ya Kazi inafanya tathmini ya ajira hizo na kudhibiti utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni. Kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Namba 10 ya mwaka 2023, asilimia 90 ya ajira zinatakiwa kwenda kwa wazawa na asilimia 10 kwa wataalamu wa kigeni.

Tathmini hiyo hufanyika kupitia ukaguzi wa kazi, uhakiki wa mikataba ya ajira na ushirikiano na taasisi kama Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa).

Kuhusu mchango wa miradi kwa wananchi wa maeneo husika, Shariff amesema muswada wa sheria ya SRC upo katika hatua za mwisho kabla ya kuwasilishwa Barazani, ambapo utatoa mwongozo wa namna wawekezaji watakavyorejesha faida kwa jamii.

Amesema kuna mjadala wa kuainisha kati ya asilimia moja hadi mbili ya faida ya mwaka wa kampuni kupelekwa kwa wananchi wa eneo husika.

Akizungumzia miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), Waziri amesema Serikali hutoa ruzuku maalum kama ahueni za kodi, ardhi au miundombinu kwa gharama nafuu, kurahisisha vibali na kutoa mikataba ya muda mrefu ili kuvutia uwekezaji na kuhakikisha jamii inanufaika.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman, alihoji msingi wa kisheria wa kubakiza asilimia ya faida kwa wananchi, huku Fatma Ramadhan Mohamed akihoji vigezo vya kumpatia mwekezaji ardhi au miundombinu bure.

Akijibu, Shariff amesema vigezo hutegemea aina ya mradi na wakati mwingine mwekezaji hupewa majengo yaliyokamilika ili kuendeleza shughuli za maendeleo kwa manufaa ya jamii na uchumi wa taifa.