Wakongwe: Manula amerudi, wengine wajipange vizuri!

AISHI Manula amerudi na moto na ni kama vile anaitaka namba yake, jambo lililowafanya hata makipa wa zamani akiwamo Benjamin Haule na Ivo Mapunda kukiri kwa kiwango alichoncho makipa wengine hasa waliopo timu ya taifa, Taifa Stars wajipange vyema, la sivyo itakula kwao.

Manula aliyerejea Azam FC baada ya kuondoka klabuni hapo tangu mwaka 2017 na alikuwa na msimu mbaya mwishoni ikiwamo kukalishwa benchi msimu mzima uliopita ameonyesha kiwango kikubwa akiwa langoni na kuwaaminisha makipa wa zamani kuamini jamaa anaenda kurejesha jina lake maarufu la ‘Tanzania One’.

Akizungumza na Mwanaspoti, kipa wa zamani wa Yanga, Polisi Morogoro, Ruvu Shooting na Lipuli, Benjamin Haule alisema Manula ameanza kurejesha kiwango bora kitakachomrejeshea jina hilo ambalo lilimkaa kwa muda mrefu alipokuwa Simba.

“Manula ndiye alikuwa Tanzania One, lakini baada ya kupata majeraha jina hilo lilipotelea mikononi mwake, wamekuja makipa wengine timu ya taifa, Taifa Stars kama Metacha Mnata, Hussein Masalanga, Yakoub Suleiman, Zuberi Foba na wengine,” alisema Haule.za:

“Tofauti yao na Manula akiwa katika kiwango, mwenzo anakuwa tegemeo kuanzia katika timu anayoichezea na Stars, mfano Masalanga hawezi kumweka nje Djigui Diarra pale Yanga wala Yakoub kumweka nje Moussa Camara kabla hajaumia, ingawa sasa ina kipa mgeni mwingine.”

Manula alipokea jina hilo kutoka kwa Juma Kaseja aliyetamba kuanzia miaka ya 2000 alipojiunga na Simba akitokea Moro United, na kipa huyo wa Azam alilitendea haki kwani 2015-2016 alinyakua tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu akimmwaga Beno Kakolanya aliyewania naye.

Msimu uliofuta wa 2016-2017 akiwa Azam alitetea tuzo hiyo akicheza mechi 28 na kukosa moja dhidi ya Mbao FC mzunguko uliokuwa umepigwa Uwanja wa CCM Kirumba na hata alipojiunga na Simba 2017-2018 aliiendelea kunyakua tuzo.

Akizungumzia moto wa Manula, kipa aliyecheza naye Azam FC licha ya kutamba na Prisons, Yanga, Simba na Taifa Stars kabla ya kwenda St George ya Ethiopia na Gor Mahia ya Kenya, Ivo Mapunda alisema: “Manula ni kipa mzuri akiwa fiti ana mwendelezo wa kiwango chake, sina maana makipa wengine ni wabaya ila wanapaswa kupambana zaidi.”

Kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ alisema: “Manula akiwa katika kiwango cha juu ni king’ang’anizi sio rahisi kuwaachia nafasi wengine na Tanzania One ilipotelea mkononi mwake na inakwenda kurejeshwa mikononi mwake.”

Jina la Tanzania One liliasisiwa miaka ya 1980 na Idd Pazi akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars akilinganishwa na Mkenya Mahmoud Abbas aliyekuwa Kenya One.