Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz amesema anaamini taasisi za Serikali zimeimarika vya kutosha na kuwapa wawekezaji imani katika kuwekeza miradi mikubwa nchini Tanzania.
Amesema hata kama kunaweza kuwepo na siasa zisizotabirika, lakini sera na mifumo thabiti iliyowekwa inatosha kujenga uaminifu kwa miaka mingi zaidi.
Rostam amebainisha hayo katika makala iliyochapishwa kwenye Jarida la The Economist kufuatia mahojiano yake na mwandishi wa makala hayo, Tom Gardner, aliyemtembelea ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.
Makala hayo yaliyochapishwa Februari 10, 2026, yanaeleza kuwa bilionea huyo mwenye asili ya Uajemi, amesema kwa kuwa biashara binafsi zilidhibitiwa vikali kwa miongo kadhaa baada ya uhuru mwaka 1961, nchi imekuwa ikijaribu kufikia washindani wake kama Kenya, ambako uwekezaji wa kigeni ulikaribishwa mapema.
Sasa, anadai, Tanzania inatoa mazingira huru na tulivu zaidi ya uwekezaji kuliko washindani wake. Anatarajia Pato la Taifa (GDP) la Tanzania kulipiku la Kenya ndani ya muongo ujao.
Rostam amemmwagia sifa Rais Samia Suluhu Hassan akimlinganisha na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Thatcher.
Kwa mujibu wake, chini ya Rais Samia, miradi mikubwa ya kimkakati kama ule wa Dola 42 bilioni za Marekani wa kugeuza gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) uliochelewa kwa muda mrefu, sasa unapiga hatua kwa kasi zaidi.
Rostam ambaye ni mwekezaji mkubwa katika sekta za madini, utalii na mawasiliano, akivuka mipaka hadi Kenya, amelieleza The Economist matumaini yake kuwa Tanzania, akipanga hoja moja baada ya nyingine kuelezea namna uchumi wake unavyozidi kuimarika kila siku.
“Hakika, Tanzania ina sababu za kuwa na matumaini. Viashiria vya uchumi mpana vinaonekana vyema: mfumuko wa bei ni wa wastani na deni la umma linadhibitika.
“Nchi pia inaweza kunufaika na ushindani unaokua kimataifa katika rasilimali za Afrika. Uamuzi wa mwisho wa uwekezaji katika mgodi mkubwa wa nikeli uliosubiriwa kwa muda mrefu unatarajiwa kufanyika mwaka huu,” ameeleza.
Gardner ameandika kwamba chama tawala nchini kinakabiliwa na mtikisiko mkubwa wa uhalali wake katika miaka 65 ya utawala wake.
Hata hivyo, Rostam anaeleza kuwa bado haijawa wazi kama Rais Samia amefanikiwa kubadili kwa kina mazingira magumu ya biashara yanayolalamikiwa kwa muda mrefu.
Anaongeza kuwa wawekezaji wa kigeni bado wanalalamikia madai ya kodi yasiyotabirika. Kuhusu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya uchaguzi, amesema hakuna uasi kwa wananchi na kwamba, Serikali imechukua hatua mbalimbali kurejesha na kujenga umoja nchini.
Amesema kwa miaka mingi, hoja ya matumaini kwa Tanzania imejengwa juu ya taswira ya utulivu wa kisiasa.