Familia ya Rais Edgar Lungu yapata pigo jingine

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku 251 tangu kifo cha Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu huku mwili wake ukiwa bado haujazikwa, Serikali ya Zambia imemnyang’anya mwanaye Dalitso Lungu, mali zenye thamani ya Sh3.37 bilioni, yakiwamo magari 79.

Lungu aliongoza Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu na Rais wa sasa, Hakainde Hichilema.

Alifariki dunia Juni 5, 2025, lakini mazishi yake yamekwama kutokana na mzozo kati ya familia na Serikali kuhusu mahali na utaratibu wa mazishi.

Tofauti na Lungu, Michael Sata alizikwa baada ya siku 14, Rupiah Banda siku saba na Kenneth Kaunda siku 20.

Wakati mwili wa Lungu ukiwa bado haujazikwa, Mahakama Kuu ya Zambia kupitia Kitengo cha Makosa ya Kiuchumi na Kifedha, Februari 9, 2026, imeamuru mali za mwanaye Dalitso Lungu na kampuni yake ya Saloid Traders Limited kutaifishwa na kuhamishiwa serikalini kwa maelezo kuwa, hazina uhalali wa kisheria.

Waendesha mashtaka wa Serikali wamechapisha kwenye ukurasa wao wa Facebook picha kadhaa zikionyesha mali zilizotaifishwa za Dalitso Lungu, zikiwamo kituo cha mafuta kinachodaiwa kuwa sehemu ya mali hizo.



Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Lusaka Times ya Zambia na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), uamuzi huo umetolewa chini ya utaratibu wa Non-Conviction Based Forfeiture, kwa mujibu wa Sheria ya Mapato Yatokanayo na Uhalifu (Proceeds of Crime Act), Kifungu cha 31.

Tathmini rasmi ya Februari 2026 imeonesha kuwa mali zinazohusishwa na Dalitso zina thamani ya zaidi ya fedha ya Zambia ZMW milioni 24 (Sh3.37 bilioni).

Pia, Mahakama imeamuru magari 79 yaliyokuwa yakimilikiwa na Dalitso yataifishwe kuwa mali ya umma, yakiwamo magari ya kifahari aina ya Rolls Royce, Mercedes-Benz, Ferrari na Lamborghini, ambayo amekuwa akionekana nayo katika maeneo ya kifahari ya Lusaka na hata Afrika Kusini.

Mbali na magari hayo, Mahakama pia imetaifisha mali zisizohamishika 23 zikiwamo za jengo la biashara na kituo cha mafuta vilivyopo Jack Compound jijini Lusaka, fleti za kifahari za ghorofa mbili na makazi ya hadhi ya juu katika eneo la Salama Park, nyumba sita katika maeneo ya Ibex Hill na Silverest, pamoja na mali nyingine katika mitaa ya Riverside na Parklands katika eneo la Copperbelt na vipande mbalimbali vya ardhi na miradi ya uendelezaji wa majengo.

Katika hukumu hiyo, nyumba moja pekee iliondolewa kwenye orodha ya mali zilizotaifishwa baada ya kubainika kuwa ilikuwa zawadi kutoka kwa baba yake.

Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa mapato ya Dalitso Lungu katika maisha yake ya ajira, ikiwamo alipofanya kazi katika Mamlaka ya Mapato ya Zambia (ZRA) na Kampuni ya Varun Beverages, yalifikia takribani ZMW 137,000 (Sh18.6 milioni).

Kiwango hicho, kwa mujibu wa Mahakama, hakiendani na umiliki wa mali zenye thamani ya mamilioni ya kwacha alizokuwa nazo.

Uchunguzi uliofanywa dhidi yake na kampuni yake ya Saloid Traders Limited ulionesha kuwa marejesho ya kodi pamoja na kumbukumbu za miamala ya benki hazikuonesha uwezo wa kifedha unaolingana na thamani ya mali zilizotajwa.

Mahakama ilitupilia mbali utetezi wake kwamba baadhi ya mali hizo zilikuwa zawadi kutoka kwa wazazi wake au zilitokana na mapato ya kilimo cha kibiashara, ikisema madai hayo hayakuungwa mkono na ushahidi wa nyaraka.

“Mahakama imebaini kuwa, Dalitso Lungu hakuwa na chanzo halali cha mapato kinachoweza kueleza umiliki wa mali hizo. Kwa msingi huo, mali hizo zinahesabiwa kuwa mapato yatokanayo na uhalifu na zinataifishwa,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Mbali na mali zilizotajwa katika hukumu hiyo, mamlaka za Zambia zimeeleza kuwa, zinaendelea kufuatilia mali nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Dalitso nchini Afrika Kusini na Dubai kwa lengo la kuzifungia au kuzitaifisha kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Wakati huohuo, timu yake ya wanasheria imetangaza kuwa inapanga kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.