Pacome, Okello wawekewa Sh 1.2Bilioni kwa sharti hili!

YANGA inaitaka robo fainali. Mabosi wa Yanga wameonyesha hawataki mchezo katika msako wa tiketi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia Kundi B, baada ya kuongeza mzigo wa maana mezani kwa wachezaji ili kuizima JS Kabylie ya Algeria.

Awali, wiki iliyopita mastaa wa Yanga waliwekewa Sh1 bilioni ili kuiua FA Rabat ya Morocco, lakini mechi hiyo iliisha kwa kupoteza bao 1-0.

Lakini, kwa sasa ipo hivi; Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wameongeza dau kama njia ya kuwatia hasira mastaa wake ili waizime JS Kabylie katika mechi ya kundi B itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mabosi wa klabu hiyo kongwe na watetezi wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho na Kombe la Muungano, wamewaahidi wachezaji wa timu hiyo kugawana Dola 450,000 (takriban Sh1.2 bilioni) endapo watafanikiwa kufuzu robo fainali.

Yanga ikiwa na mastaa wote wakiwamo Pacome Zouzoua na Allan Okello itaikaribisha JS Kabylie, Jumapili katika mechi ya mwisho ya kufungia hatia ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, japo itakuwa pia ikiombea FAR Rabat ya Morocco ipoteze mbele ya Al Ahly ya Misri zitakazoumana pia siku hiyo jijini Cairo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba, mabosi wamekubaliana na kikosi chao kugawana nusu ya zawadi ya Dola 900,000 inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa timu inayofuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

“Tumeahidi kwamba wachezaji watapata nusu ya fedha tutakazopokea kutoka CAF iwapo tutafuzu robo fainali,” alisema kiongozi mmoja mwandamizi wa klabu hiyo (jina tulihifadhi).

 “Tunafahamu kuwa kufuzu kwetu kutategemea si tu matokeo yetu, bali pia matokeo ya mechi kati ya Al Ahly na FAR Rabat.”

Kwa Yanga, hesabu za kufuzu ni wazi iwapo itashinda idadi ya mabao yasiyopungua 2-0, huku FAR Rabat wakipasuka, kwani kwa sasa wanatofautiana pointi, Wamorocco wakiwa na nane, ilhali Yanga tano.

Kama Yanga itashinda itafikisha pointi nane na uamuzi wa timu ya kuungana na Al Ahly utategemea uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, matokeo ya jumla baina yao ni 1-1, kila moja ikishinda nyumbani kwake bao 1-0.

Iwapo Al Ahly na ASFAR watatoka sare, Yanga wataondolewa moja kwa moja katika michuano hiyo ikiwa ni mara ya pili mfululizo kwani msimu uliopita ilikwama ikiwa na pointi nane, bila kujali watashinda kwa mabao mangapi dhidi ya JS Kabylie.

Hali hiyo inaonyesha jinsi ushindani ulivyo mkali katika hatua ya makundi.

“Kwenye soka lolote linaweza kutokea,” alisema kiongozi huyo.

“Bado tuna nafasi na wachezaji wanaelewa kinachotakiwa. Motisha ipo.”

Mbali na motisha ya kifedha, kufuzu kuna mafanikio makubwa kimchezo kwa Yanga na kuimarisha hadhi ya klabu kama moja ya timu mahiri Afrika, sambamba na kuthibitisha uwekezaji uliofanywa hivi karibuni katika kuongeza ubora wa kikosi.

Maandalizi ya mechi hiyo tayari yanaendelea. Baada ya safari ndefu na ngumu kutoka Morocco, wachezaji walipewa muda wa kupumzika kabla ya kurejea mazoezini.

“Baada ya safari ndefu, wachezaji walipumzika kwanza,” alieleza kiongozi huyo.

“Mazoezi yalianza tena jana (juzi) huku tukianza maandalizi ya mwisho ya mechi.”

Kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves anaendelea kukuna kichwa kusaka mbinu za kuivusha Yanga kwenda robo fainali  baada ya kuteleza kwa kupoteza mbele ya AS FAR Rabat bao 1-0 na kutoka sare ya 1-1 nyumbani mbele ya Al Ahly iliyowafunga awali kwa mbo 2-0 ugenini.

Yanga ilianza hatua ya makundi kwa kishindo kwa kuinyuka AS FAR Rabat kwa bao 1-0 kisha kwenda kutoka suluhu na JS Kabylie ugenini, lakini ikapoteza kwa Al Ahly ugenini kabla ya kutoka sare nyumbani na kuifanya ikusanye pointi tano ilizonazo hadi sasa ikishika nafasi ya tatu katika kundi.