Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila, amesema mkoa hauwezi kubaki na taswira ya zamani na lengo la Serikali ni kuufanya kuwa wa kisasa. Akizungumza Februari 11, 2026, katika ziara ya kukagua ujenzi wa barabara na madaraja wilayani Kinondoni, Chalamila amewaonya makandarasi wanaosuasua ujenzi wa miradi ikiwemo barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT 4), kipande cha kwanza mjini hadi Mwenge na cha pili kutoka Mwenge kuelekea Tegeta.
Mradi wa kipande cha kwanza wenye thamani ya Sh174.3 bilioni, unaotekelezwa na kampuni ya China Geo Engineering, ulitakiwa kukamilika Aprili 2025 lakini uko nje ya muda na sasa unapangwa kumalizika Juni 15, 2026. Hadi Januari 2026, ulikuwa umefikia asilimia 47 tu, huku ulitakiwa kufikia asilimia 65. Chalamila ametoa wiki mbili kwa makandarasi wote na kuwataka kufanya kazi usiku na mchana.
Ameeleza kushangaa hoja za mkandarasi kwamba kazi mjini ni ngumu kuliko kijijini. “Nisipokuta mabadiliko baada ya wiki hizi mbili, hawa watalala ndani ili wajifunze umuhimu wa kukimbiza maendeleo ya Watanzania,” amesema. Amesema malighafi yote ipo, ikiwemo saruji, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha miradi, ambayo kuchelewa kwake kunawaathiri wananchi.
Pia ametoa wiki mbili kwa mkandarasi wa kipande cha pili cha Mwenge-Tegeta kumaliza mradi. Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutafanikisha azma ya Serikali ya kuboresha mundombinu wa jiji, kupunguza foleni na kuhakikisha madaraja na barabara ni ya kisasa.
Aidha, amewaonya wakazi wa Dar es Salaam wasijenge mabondeni, akibainisha kuwa matokeo mabaya ya mvua mara nyingi husababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu. Chalamila amesisitiza umuhimu wa wakazi kutumia madaraja mapya kwa miguu ili kuona tofauti na barabara za zamani.
Diwani wa Kunduchi, Michael Urio, ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja la Mtongani kutaboresha mawasiliano na shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mkoa.