Dar/Tanga. Utata umegubika kifo cha Mohamed Kisingwe (29), anayedaiwa kupoteza maisha mikononi mwa Jeshi la Polisi, baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Kinachoibua utata huo ni ukinzani uliopo katika taarifa za chanzo cha kifo zilizotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kuwa ni presha, huku familia yake, ikisema ndugu yao hakuwahi kuwa na historia ya ugonjwa huo.
Utata mwingine unatokana na simu ya marehemu kutumika kuwapigia ndugu zake na viongozi wake wa kijiji na kata, wakiulizwa jina lake kamili, jambo linaloibua swali kuwa, walimkamataje bila kumuuliza jina.
Hata hivyo, Kisingwe sio mtu wa kwanza kupoteza maisha katika mazingira tatanishi, Januari mwaka huu Michael Lambau (18), mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia kwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Moshi Kati.
Mwingine aliyepoteza maisha katika mazingira kama hayo ni Shaban Luluba, mkoani Pwani. Kifo cha Lububa cha Januari 8, mwaka huu, kilitokana na kupigwa risasi na askari polisi wakati wa operesheni ya kukamata.
Hata hivyo, Januari 8, mwaka huu Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitangaza jeshi hilo, limeanza kufanya uchunguzi wa matukio matatu likiwamo la kifo cha Joseph na Luluba, kubaini iwapo vifo vyao vilisababishwa na askari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi hilo linafanya uchunguzi huo kwa kina na kwamba hatua zote za kisheria zitachukuliwa ipasavyo iwapo kuna atakayebainika kuhusika.
Hata hivyo, uamuzi wa polisi kujichunguza mara kadhaa ulikosa uungwaji mkono kwa kuwa, bado taarifa ya uchunguzi huo haijawekwa wazi.
Februari 4, mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alimwagiza aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati kuchunguza wa mauaji yaliyodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, akisema polisi haiwezi kujichunguza yenyewe.
“Kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizopo, jeshi ndilo lililofanya mauaji. Kwa maana hiyo, taarifa niliyonayo ni kwamba, jeshi limetengeneza kamati ya kufanya uchunguzi alafu walete taarifa, haiwezekani jeshi lifanye mauaji, jeshi lijichunguze lenyewe.
“Nimemuelekeza Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi alafu watuletee taarifa, lakini wakati huo huo, nataka Jeshi lako lijitafakari waone kama kinachotokea ni misingi ya Jeshi la Polisi,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano, Februari 11, 2026 Bakari Juma ni mjomba wa Kisingwe, amesema familia imeingiwa na wasiwasi kuhusu chanzo halisi cha kifo hicho huku akiomba kufanyike uchunguzi maalumu kubaini uhalisia.
Amesema utata wa tukio hilo ulianza pale Diwani wa Mayomboni, Husein Kamoyo alipopokea simu kwa namba ya marehemu kutoka kwa watu waliojitambulisha kuwa askari polisi na kuomba jina la marehemu.
“Tunafikiri wakati wanaomba majina walikuwa wameshamdhuru kwa kuwa kama alikuwa hai, ilishindikana vipi kumuuliza mwenyewe?” amehoji.
Amesema inakuaje polisi wasema amekufa kwa presha, lakini ndugu na jamaa hawakuwahi kujua kama alikuwa na ugonjwa huo, ndiyo maana wanaomba uchunguzi wa kina.
Ameeleza mwili wa marehemu bado umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo, wakisubiri taratibu za kuuchukua zikamilike.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayomboni, Mwinjimwa Ramadhan amesema alipokea taarifa za kushikiliwa kwa mwananchi wake Februari 7, 2026 na hakuwa na wasiwasi akiamini yupo kwenye mikono salama.
“Nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni polisi kutoka Duga Mtandikeni wakiniuliza kama namfahamu mtuhumiwa, nikawaambia kama wako naye wamuulize mwenyewe,” amesema mwenyekiti huyo.
Ameongeza baadaye walimpigia tena simu kumuuliza jina la mtuhumiwa na taarifa za familia yake, kisha jioni akaelezwa kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.
“Baada ya mahojiano kuhusu ndugu na shughuli zake, ndipo waliponiambia kuwa amefariki dunia,” amesema.
Kwa upande wake diwani huyo, amekiri kupigiwa simu siku ya tukio kutoka namba ya marehemu na waliotumia simu hiyo waliomba majina matatu ya marehemu.
“Walijitambulisha kwanza kuwa ni polisi, baadaye wakasema ni wasamaria wema, wakasisitiza niwape majina ya marehemu.
“Nilipowauliza kama amepata ajali ya aina gani na kwa nini wasimpeleke hospitali kama hali ni mbaya, hawakunipa maelezo ya kina,” amesema Kamoyo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi imeeleza kuwa, Kisingwe alifariki dunia akidaiwa kuwakimbia maofisa wa askari wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) waliokuwa wakimkamata.
“Tukio lilitokea Februari 7, 2026 baada ya maofisa wa DCEA kupata taarifa za watu waliokuwa wakisafirisha mirungi katika eneo la Mahandakini, Mayomboni,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Amesema maofisa hao walimwona mtu akiendesha pikipiki namba MC 723 EFD inayodaiwa kubeba mirungi, ambaye alisimamisha pikipiki na kukimbia kabla ya kukamatwa.
“Baada ya kukamatwa alionekana kuhema kwa shida na kuchoka sana, hivyo alipelekwa hospitalini ambako alifariki dunia; uchunguzi wa awali unaonesha kifo kilitokana na kushuka kwa presha,” amesema.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.