Na WAF, Dar es Salaam
Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba Asili imepeleka timu ya wataalam mkoani Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa huo kwa lengo la kuwasajili waganga wa tiba asili.
Timu hiyo inaendesha zoezi la usajili kuanzia tarehe 09 hadi 20 Februari, 2026 katika Mtaa wa Mkunguni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa zoezi hilo, Bi. Lucy Laurian, amesema lengo la usajili huo ni kuhakikisha waganga wote wa tiba asili wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
“Tunawahimiza wataalam wote wa tiba asili kujitokeza kwa wingi kujisajili ili wapate vibali halali vya utoaji huduma. Kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Sura ya 244 ya Sheria za Tanzania, ni kosa kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili bila kusajiliwa na Baraza,” amesema Bi. Laurian.
Ameongeza kuwa kifungu cha sheria hiyo kinampa mamlaka Msajili na Baraza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote anayekiuka masharti ya usajili, ikiwemo kutozwa faini au kuchukuliwa hatua nyingine kwa mujibu wa sheria.
Wizara ya Afya imesisitiza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha na kurasimisha huduma za tiba asili nchini, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, zenye viwango na zinazotambuliwa kisheria.

.jpeg)
.jpeg)