Rais Samia safarini Ethiopia kushiriki mkutano AU  

Dar es Salaam. Katika siku 101 tangu alipoapishwa kuiongoza Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya safari mbili za nje ya nchi, ikiwa ni mikakati wa kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia.

Safari ya kwanza, aliifanya Februari 2, 2026, alikokwenda Falme za Kiarabu (UAE), kushiriki Jukwaa la Afrika la Uwekezaji Duniani (GAIS), akikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa ulimwengu.

Mkuu huyo wa nchi, aliapishwa Novemba 3, 2025 kuitumikia Tanzania kwa muhula wa pili, baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Ukiacha safari alizofanya nje ya Tanzania, tayari ndani ya siku hizo, Rais Samia ametembelewa na Mkuu wa nchi mmoja, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Februari 7, 2026.

Ukiacha ziara ya Museveni, Rais Samia pia amepokea ugeni kutoka uwakilishi wa mataifa mbalimbali, ingawa hawakuwa wakuu wa nchi.

Taarifa ya safari hiyo ya Ethiopia imetolewa leo, Alhamisi Februari 12, 2026 na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia, ameondoka nchini leo Alhamisi, Februari 12, 2026 kuelekea Addis Ababa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa 39 wa AU, utakaofanyika kwa siku mbili Februari 14 na 15.

Kabla ya mkutano huo, taarifa inaeleza Februari 13, atashiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto.

Baadaye, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Samia atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Rais Samia pia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Russell Dlamini, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Sidi Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.

“Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika utaongozwa na Kaulimbiu ya mwaka 2026 inayosema, ‘Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeeleza kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza hatua za pamoja za bara katika kuhakikisha usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii, na maendeleo endelevu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam  Februari 12, 2026 kabla ya kuondoka nchini kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).



Tanzania inakamilisha muda wake wa kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika baada ya kulitumikia kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, hivyo kutoa mchango katika kuimarisha amani, utulivu na usalama barani Afrika.

Sambamba na masuala mengine, imesema mkutano huo utatangaza rasmi uongozi wa AU kwa mwaka 2026 na Jamhuri ya Burundi itachukua nafasi ya uenyekiti, huku Tanzania ikiteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, ikiwakilisha Kanda ya Mashariki, nafasi inayoakisi imani ya nchi wanachama kwa mchango na uongozi wa Tanzania katika masuala ya Bara la Afrika.

Aidha, katika mkutano wa mwaka huu, Rais Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa kinara wa AU katika masuala ya afya ya mama na mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi katika mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali.

“Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia, na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika,” imeeleza taarifa hiyo.

Kupitia ushiriki wake katika mkutano huo, taarifa hiyo imeeleza Tanzania inalenga kuendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa, kutetea masilahi ya Taifa na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano, uthabiti wa kiuchumi na maendeleo endelevu.