Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura ametaja maeneo matatu yanayopaswa kusimamiwa kwa umakini katika kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuondoa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndani ya jeshi hilo.
Maeneo hayo ni utunzaji wa vielelezo, usimamizi wa mali za kuokota pamoja na utunzaji wa daftari la mali za jeshi, watumishi hao wanapaswa kuongeza umakini katika maeneo hayo ili kuepuka kuisababishia taasisi hasara.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wanadhimu na wahasibu wa Jeshi la Polisi, kilicholenga kuimarisha nidhamu ya matumizi ya rasilimali za fedha za umma na mifumo rafiki kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza leo, Alhamisi Februari 12, 2026, katika hafla iliyofanyika Shule ya Polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro, IGP Wambura amesema anatambua jitihada zinazofanyika kuondoa hoja za wakaguzi wa ndani na nje, huku akiwataka watumishi kuacha matumizi yasiyo na tija, kuheshimu fedha za umma.
“Kwa muktadha huo, utunzaji wa vielelezo, mali za kuokota na daftari la mali ni maeneo ninayowaelekeza mkayafanyie kazi kwa nguvu zote ili kuhakikisha ubora wa utendaji unaimarika,” amesema.
Amesema hata matumizi madogo yasiposimamiwa vizuri yanaweza kusababisha hasara kubwa. “Tuwe makini na matumizi madogomadogo, kwa kuwa tundu dogo linaweza kuzamisha meli kubwa. Umakini unahitajika katika usimamizi wa fedha za taasisi ili kuepuka hasara.”
Amewataka maofisa hao kuboresha mifumo ya malipo ili iweze kusomana kwa kuzingatia mwelekeo wa Serikali, pamoja na kuendelea kujifunza ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
IGP Wambura amesema viongozi wanapaswa kuwa mfano wa maadili mema, akisisitiza maadili duni katika ngazi ya juu huigwa na watendaji wa ngazi za chini.
“Maadili ya juu yanapaswa kuanzia kwenu ili iwe rahisi kuwasimamia watendaji wa ngazi za chini katika kusimamia fedha na rasilimali watu,” amesema.
Pia, amewataka kusimamia kwa uadilifu rasilimali za taasisi, zikiwemo magari yaliyotolewa na Serikali, hasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Tumepata rasilimali nyingi kuanzia mwaka 2022 hadi sasa, na bado tunaendelea kupata. Niwaombe tusimamie mali hizi za Serikali kwa umakini,” amesema.
Hata hivyo, IGP Wambura ameonyesha matumaini kutokana na mabadiliko ya kimtazamo na kifikra ndani ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
“Kuna miradi mingi inaendelea na thamani ya fedha inazingatiwa. Aina na ubora wa majengo yanayojengwa vinaonekana. Ingawa mimi si mhasibu, nimewahi kuona majengo mabovu yenye thamani kubwa ya fedha,” amesema.
Ametaja baadhi ya maeneo yenye miradi ya ujenzi wa ofisi za makamanda wa polisi inayotekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha kuwa ni Simiyu, Mtwara, Rufiji na Songwe.
“Lakini hata Mkuranga, ambako thamani ya fedha iliwahi kupotea mwaka mmoja uliopita, sasa jengo linakaribia kukamilika na unaona thamani ya fedha. Tulipofika tuendelee mbele,” amesema.
Kwa upande wake, Kamishna wa Fedha na Lojistiki wa taasisi hiyo, Liberatus Sabas amesema kikao kama hicho kinafanyika kila mwaka na lengo lake kuwakumbusha wahasibu katika majukumu yao ya usimamizi wa raslimali fedha na vifaa.
“Tunakumbushana na kujenga uelewa wa pamoja juu ya usimamizi bora wa raslimali fedha unaojumuisha utendaji unaozingatia taratibu za malipo, manunuzi, na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali,”amesema
Amesema katika mkutano huo wataangazia bajeti ya jeshi hilo, ulipaji mishahara ya watumishi wake na maandalizi ya kustaafu watumishi, huku akisema mwaka uliopita walipata hati inayoridhisha kutoka kwa CAG.
“Waliotufanya tupate hati hiyo ni hawa hapa, utakuwa shahidi wakati unaingia madarakani kulikuwa na hekaheka nyingi za matumizi sahihi ya fedha za umma maneno mengi yalisemwa baada ya kaguzi maeneo mbalimbali ya Jeshi la Polisi,” amesema.
Sabas amesema hadi kuna wakati msemo uliibuka wa “Mbwa kala Mbwa” kutokana na mambo yalivyokuwa yanakwenda ingawa wameshatoka huko baada ya kujenga utamaduni wa kukutana kufanya tathimini.