Na MASHAKA MHANDO,Tanga
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Tanga Ijumaa February 13, ambapo atakagua na kuzindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 758.1.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, akizungumza na waandishi wa habari Leo February 12 ofisini kwake alisema Waziri Mkuu atapokelewa majira ya saa tatu asubuhi katika eneo la Mkata, Wilayani Handeni, akitokea mkoani Pwani.
Akiwa Handeni, Waziri Mkuu atakagua mradi mkubwa wa umeme utakaohudumia wilaya za Pangani, Muheza na Korogwe, kisha atazindua chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kuweka jiwe la msingi la ujenzi.
Baada ya hapo, msafara utaelekea wilayani Kilindi kukagua mradi wa tenki la maji na hospitali ya wilaya, kabla ya kuelekea Korogwe kwa ajili ya ukaguzi wa mradi mkubwa wa maji wa miji 28.
Ratiba inaonyesha kuwa Februari 15, Waziri Mkuu atakuwa wilayani Mkinga kukagua ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, kisha kuelekea Jijini Tanga kukagua maboresho ya Bandari ya Tanga na kuzungumza na wananchi katika viwanja vya CCM Masiwani, eneo la Lamore.
Februari 16, Waziri Mkuu atakagua mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) eneo la Chongoleani na viwanda vya mifuko, kisha kuelekea Pangani kukagua daraja la mto Pangani na Muheza kukagua jengo la Halmashauri.
Februari 17, Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake wilayani Lushoto kwa kuweka jiwe la msingi katika hoteli ya kitalii ya Java Boutique Hotel, pamoja na kuzindua kituo cha kutengenezea Oxygen katika hospitali ya wilaya na kukagua shule ya Amali Mlalo kabla ya kuelekea mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Wazee mkoa wa Tanga, Shekue Pashua na Mjumbe wa Kamati ya Amani, Mchungaji Elizabeth Bayo, kwa nyakati tofauti wamesema watampokea kwa mikono miwili, wakisisitiza kuwa uwekezaji wa bilioni 700 ni faraja kubwa kwa uchumi wa Tanga uliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.



