Pwani. Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wanatarajiwa kunufaika na maboresho ya huduma za kijamii, ikiwemo elimu, afya na miundombinu, kufuatia Baraza la Madiwani kupitisha bajeti ya Sh76.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Bajeti hiyo inayotokana na mapato ya ndani, ruzuku kutoka Serikali Kuu pamoja na michango ya wahisani, imepitishwa leo Alhamisi, Februari 12, 2026, katika kikao cha baraza kilichofanyika wilayani humo.
Kiasi hicho ni ongezeko la Sh8,455,866,165 ikilinganishwa na bajeti ya Sh67,879,797,904 iliyopitishwa kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2025/2026, hali inayoonyesha kuimarika kwa uwezo wa kifedha wa halmashauri hiyo katika kugharamia miradi ya maendeleo.
Madiwani wa baraza la Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye kikao cha bajeti, Picha na. Sanjito Msafiri
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo, Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ismail Bilali, amesema fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya vipaumbele, ikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu na kuinua uchumi wa wananchi.
Amesema lengo ni kuhakikisha huduma za msingi zinaboreshwa na kuwafikia wananchi kwa ufanisi, sambamba na kusimamia matumizi ya fedha kwa kuzingatia thamani ya fedha ili miradi inayopangwa itekelezwe kwa ubora na kwa wakati.
Akizungumza baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Leon Mgweno, amesema baraza limejipanga kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mipango yote ili malengo yaliyowekwa yafikiwe.
“Tumejipanga kuhakikisha bajeti hii inatekelezwa kikamilifu, miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Chalinze,” amesema Mgweno.
Madiwani wa baraza la Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye kikao cha bajeti, Picha na. Sanjito Msafiri
Baadhi ya madiwani waliochangia mjadala wa bajeti hiyo, akiwamo Selestini Semiono wa Kata ya Msata na Juma Gurumo wa Kata ya Kimange, wamesema mpango huo wa matumizi ya fedha utaleta nafuu kwa wananchi kwa kuwa umejikita katika kuboresha huduma muhimu na kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
Gurumo amesisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa miradi ili fedha zilizoidhinishwa ziwe na matokeo yanayoonekana katika sekta za elimu, afya na miundombinu ya ndani.
Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ilianzishwa mwaka 2013 baada ya kugawanywa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ikiwa na dhamira ya kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi.
Tangu kuanzishwa kwake, imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya, uboreshaji wa barabara za ndani pamoja na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta za kilimo, biashara na elimu.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatarajiwa kuimarisha kasi ya utekelezaji wa miradi mipya na kukamilisha inayoendelea, hatua itakayochangia kuboresha ustawi wa wananchi wa Chalinze katika mwaka ujao wa fedha.