Hanang. Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mathew Kundo, amewataka watendaji wa sekta ya maji nchini kutumia mifumo ya kiteknolojia kubaini na kudhibiti upotevu wa maji, sambamba na kusimamia viwango na ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miradi ya maji ili kuboresha huduma kwa jamii.
Mhandisi Kundo ametoa maelekezo hayo leo, Alhamisi, Februari 12, 2026, katika mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang’ mkoani Manyara, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Gharama za Uwekezaji wa Huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH), unaokadiriwa kugharimu Sh94.62 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano.
“Watendaji wa sekta ya maji mnapaswa kutumia mifumo ya kiteknolojia ili kubaini na kudhibiti upotevu wa maji na kuboresha huduma kwa jamii,” amesema Mhandisi Kundo.
Amesema mpango huo umeainisha hali ya sasa ya huduma, mahitaji yaliyopo, malengo yanayotarajiwa kufikiwa na rasilimali zitakazohitajika ili kuhakikisha wananchi wa Hanang’ wanapata maji safi na salama, vyoo bora na mazingira yenye usafi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla, kuimarisha ufanisi wa taasisi za maji na kuziba mianya ya upotevu, ikiwamo mivujo.
Naibu Waziri wa Maji mhandisi, Mathew Kundo (kushoto) akimkabidhi mbunge wa Hanang’, Asia Halamga, nakala ya mpango wa gharama za uwekezaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (Wash) uliofanyika mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang’ mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Pia amesema serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa Gridi ya Maji ya Taifa kwa lengo la kuongeza uhakika wa upatikanaji wa maji nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema mpango huo wa uwekezaji wa WASH ni ramani ya utekelezaji iliyoandaliwa kwa kuzingatia ushahidi na gharama halisi, sambamba na kuendana na vipaumbele vya kitaifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6).
Amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea uongozi thabiti wa serikali na ushiriki wa wadau wote, wakiwamo wananchi wa eneo husika.
“Sisi kama WaterAid Tanzania, tupo tayari kuendelea kutoa msaada wa kitaalamu na kushirikiana kwa karibu na serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” amesema Mzinga.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030, uwekezaji unaohitajika ni wa Sh94.62 bilioni. Maeneo ya kipaumbele ni huduma za maji (asilimia 36), huduma za WASH shuleni (asilimia 35), vituo vya kutolea huduma za afya (asilimia 13), usafi wa mazingira katika kaya pamoja na usimamizi wa majitaka na taka ngumu (asilimia 12) na huduma za WASH katika maeneo ya umma (asilimia nne).
Mzinga amesema tangu mwaka 1983, WaterAid Tanzania imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali kuchangia juhudi za serikali kuhakikisha kila mtu na kila mahali yanapatikana maji safi, vyoo bora na huduma za usafi binafsi.
Amesema hadi sasa zaidi ya watu milioni 8.5 wamefikiwa na miradi ya taasisi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Alimishi Hazali, amesema mradi wa WASH una umuhimu mkubwa katika kumaliza changamoto za maji mashuleni, vituo vya afya na majumbani.
“Natoa wito kwa wadau wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, jamii na vyombo vya habari kuunga mkono utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha maji safi na salama, vyoo bora na huduma za usafi zinapatikana kwa kila mtu, kila mahali Hanang’ ifikapo mwaka 2030,” amesema Hazali.
Mbunge wa Hanang’, Asia Halamga, ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji wilayani humo. Amesema utekelezaji wa mpango huo utaleta mageuzi makubwa katika huduma za maji na ustawi wa wananchi.
Naye mkazi wa Katesh, Alexander Bayo, ameishukuru serikali na WaterAid Tanzania kwa kufanikisha mpango huo, akisema umeongeza tija kwa jamii katika upatikanaji wa maji na huduma za usafi.
Amesema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa eneo hilo na kuiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuendelea kuwekeza katika miradi itakayochochea maendeleo ya Hanang’.