Kwa hili JKT Tanzania kiboko

LICHA ya JKT Tanzania kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ikiongoza kwa pointi 27, kikosi hicho cha maafande ndio kinachoongoza kwa wachezaji wa timu hiyo kuonyeshwa kadi nyekundu, kuanzia msimu wa 2024-2025 hadi sasa 2025-2026.

Tangu kuanza msimu wa 2024-2025 hadi sasa 2025-2026, tayari wachezaji wa JKT Tanzania wameonyeshwa kadi nyekundu tano za Ligi Kuu Bara, wakifuatiwa na TRA United na Pamba Jiji ambazo kila mmoja zimepata nne, ikifuatiwa na KMC iliyopata tatu.

Kwa msimu wa 2024-2025, nyota wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu kwa JKT Tanzania alikuwa ni kipa, Denis Richard, katika kichapo cha timu hiyo cha mabao 2-0, dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga, mechi ikipigwa, Oktoba 22, 2024.

Nyota mwingine aliyefuatia msimu huo ni Mohamed Bakari, katika kichapo pia cha kikosi hicho cha bao 1-0, dhidi ya Simba, lililofungwa kwa penalti na Jean Charles Ahoua dakika ya 90+5, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Desemba 24, 2024.

Kwa msimu huu wa 2025-2026, nyota watatu wameonyeshwa kadi nyekundu, akianza pia kipa, Ramadhan Chalamanda, katika mechi dhidi ya timu ya Mbeya City iliyopigwa Oktoba 24, 2025, huku ikishuhudia miamba hiyo ikitoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Mwingine ni Salum Khamis, katika kichapo cha timu hiyo cha bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Januari 30, 2026, ikiwa ni mwendelezo mbaya kwa nyota wa kikosi hicho cha maafande.

Nyota wa mwisho aliyeonyeshwa kadi nyekundu ni beki wa kushoto, Karimu Mfaume, katika ushindi wa kikosi hicho wa bao 1-0, dhidi ya maafande wenzao wa Mashujaa FC, Februari 9, 2026, hivyo, kufikisha wachezaji watano tangu msimu uliopita.