MSHAMBULIAJI Kibu Denis aliyekuwa Simba aliyelamba dili la kujiunga na Al Nasr Benghazi ya Libya ameshindwa kujizuia wakati anasepa zake kwa kuwaambia mashabiki wa klabu hiyo kwamba, kwa mziki unaoshushwa na kocha Steve Barker hivyo wajiandae kushuhudia sapraizi Msimbazi.
Kibu aliyejiunga na Simba mwaka 2021 akitokea Mbeya City ameuzwa Al Nasr baada ya kulamba dili la mkataba wa muda wa miezi mitano, lakini lenye donge nono ambalo hata hivyo limefichwa kwa sasa, huku akiwa mmoja ya nyota waliokuwa muhimu katika kikosi hicho cha Msimbazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kibu alisema ndoto ya kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa miaka mingi imetimia kwa kujiunga na Al Nasr na kwamba ataenda kupambana na kuonyesha ni kwa namna gani alitamani, huku akikichambua kikosi kilichopo Msimbazi chini ya kocha Barker akisema anakitabiria kuwasapraizi mashabiki mwishoni mwa msimu huu.
Kibu aliyeifungia Simba jumla ya mabao 15 katika misimu minne na nusu tangu 2021, alisema Simba ya sasa ina wachezaji bora na wenye vipaji na chini ya kocha Barker anaiona ikifika mbali licha ya changamoto ilizopitia mwanzoni mwa msimu huu.
“Simba ina wachezaji wengi bora na nimepata nafasi ya kucheza nao pamoja kuna ambao tulijiunga nao pamoja na wengine niliwakuta siwezi kumtaja mmoja mmoja nawashukuru kwa ushirikiano mzuri waliokuwa wananipa naamini wataendelea kuipambani timu ifike malengo,” alisema Kibu aliyekuwa mmoja ya nyota waliyoifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
“Simba ni timu bora sio tu Tanzania hadi Afrika imekuwa imara zaidi ndani na kimataifa, licha ya hivi sasa kupitia changamoto lakini imefanya mambo mengi makubwa naamini itarejea kwenye ushindani na kuwasapraizi wote wanaoichukulia poa,” aliongeza Kibu anayeitumikia pia Taifa Stars.
Kuhusu dili alililopata, Kibu alisema anaondoka Simba akiwa anaikumbuka kwa namna alivyofanya kazi nayo tangu atue kutoka Mbeya City na anaenda ughaibuni kama balozi wa klabu hiyo na anaomba wamuombee ili afanye kazi kwa ufanisi.
“Hii sio tu nafasi bora niliyopata ni bahati kwangu baada ya kujaribu kwa muda naamini ntaenda kupeperusha vyema bendera ya Simba na Tanzania kwa ujumla. Kucheza nje ya nchi yangu ni sehemu ya ndoto sasa ni wakati wa kwenda kuonyesha ni kwa nini nilikuwa na tamaa hiyo,” alisema Kibu.
“Simba ni nyumbani huenda nikapata riziki nyingine ya kurudi hapo baadae nawashukuru sana na nawatakia kila la kheri, natamani kusikia ikitwaa taji msimu huu hilo kutimiza malengo tuliyokuwa tumejipangia mwanzoni mwa msimu.”
Kibu alisema alikuwa na misimu minne na nusu ya furaha ndani ya Simba licha ya kushindwa kuipa taji lolote la Ligi Kuu Bara ama Kombe la Shirikisho, japo ametwaa nayo Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano 2024, alisema lakini malengo ya pamoja yalikuwa niipambania Simba kufanya vizuri ndani na kimataifa, lakini msimu huu mambo yameenda kinyume, ila ni timu bora.
Alipoulizwa kuhusu Al Nasr alisema ni kama anaenda nyumbani kwani anaenda kukutana na wachezaji zaidi ya wawili aliofanya nao kazi pamoja Simba hivyo hatakuwa mgeni anatarajia kupata ushirikiano mzuri kwa walio mtangulia ambao ni Steven Mukwala na Fabrice Ngoma.