WAKATI kikosi cha Yanga kikitarajiwa kuondoka leo Alhamisi kwenda Zanzibar kwa ajili ya mechi ya mwisho ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya kuamua hatma ya kutinga robo fainali, nyota mpya wa timu hiyo Buba Jammeh ametua na atakuwa sehemu ya msafara wa kikosi hicho.
Yanga ilimsajili Jammeh kupitia dirisha dogo lililofungwa Januari 30 mwaka huu ikiwa ni mkakati wa timu hiyo kuimarisha eneo la ushambuliaji, lakini sasa taarifa ziwafikie mashabiki winga huyo tayari yupo Dar na anaondoka na msafara wa timu kwenda Zenji.
Unaambiwa kwamba, Mgambia huyo alishakuwepo kwenye mazoezi ya mwisho ya kikosi hicho hapa Dar es Salaam kabla ya kwenda Zanzibar kwenye mechi dhidi ya JS Kabylie.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, kiungo mshambuliaji huyo alitua Bongo siku mbili kabla lakini Yanga haikutaka kumweka wazi.
“Buba ameshafika ana siku mbili sasa hapa mjini, ni vile timu ilikuwa kwenye mapumziko nadhani leo jioni (jana) atakwenda mazoezini kuanza kazi rasmi. Kocha ndiye ataamua maana timu itaondoka kesho (leo) kwenda Zanzibar sasa uamuzi utabaki kwa makocha kama wataona anaweza kuwa sehemu ya mchezo ujao ni sawa, sisi kama uongozi kazi yetu tumeshaimaliza,” kilisema chanzo kutoka klabu ya Yanga
Awali, kiungo mshambuliaji huyo alitarajiwa kujiunga na timu nchini Morocco, lakini alilazimika kurejea Gambia baada ya pasipoti yake kuisha muda wa matumizi.
“Buba amerudi na ameanza mazoezi,” kilithibitisha chanzo hicho.
“Upatikanaji wake unalipa benchi la ufundi chaguo zaidi la safu ya ushambuliaji tunapohitaji mabao.”
Buba anatua Yanga akitokea Interclube ya Angola ambayo ameichezea kwa msimu mmoja tu na kote akiingia dirisha dogo na kutoka muda huo huo, huku akiacha rekodi ya kufunga mabao manne.
Interclube msimu huu haina rekodi nzuri katika ligi ya Angola, kwani inashika nafasi ya 11, ikiwa imecheza mechi 14 ikiwa na pointi 16, huku kinara akiwa nazo 36 katika mechi 14.
Muangola huyo anakwenda kuchukua nafasi ya Moussa Balla Conte ambaye ametolewa kwa mkopo na kwenda Raja Casablanca, timu anayoifundisha kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.
Conte aliondoka kutokana na ugumu wa namba pale Jangwani. Swali ni je, Buba atatoboa mbele ya mastaa kama Pacome Zouzoua ambaye tayari ameshapenya kwenye hesabu za kocha Pedro Goncalves?
Yanga itashuka kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Jumapili hii dhidi ya JS Kabylie ya Algeria ikihitaji ushindi na kuiombea mabaya AS FAR Rabat mbele ya Al Ahly ya Misri ili ikate tiketi kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Vinara wa kundi Al Ahly, ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakilibeba taji hilo mara 12, tayari wamefuzu robo fainali lakini wanalazimika kuepuka kipigo ili wasimalize wa pili.