Dar es Salaam. Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Likwati iliyopo wilayani Temeke, Dar es Salaam, wamepatiwa mafunzo maalumu ya lishe kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandaa chakula bora kwa watoto wao na hivyo kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu.
Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uelewa wa wazazi kuhusu umuhimu wa lishe bora shuleni na nyumbani, kufuatia kubainika kwa hali isiyoridhisha ya ulaji miongoni mwa watoto, inayochangia kudumaa kwa ukuaji, matatizo ya kiafya na kushuka kwa kiwango cha ufaulu darasani.
Hatua hiyo pia inakuja wakati shule hiyo ikikabiliwa na changamoto ya ushiriki mdogo wa wazazi katika mpango wa chakula shuleni. Kati ya wanafunzi 210 waliopo, ni wanafunzi 130 pekee wanaopata chakula shuleni hapo.
Akizungumza leo Alhamisi Februari 12, 2026, Mkurugenzi wa Mafunzo na Elimu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Esther Mkuba, amesema takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya watoto walio chini ya miaka mitano nchini wanakabiliwa na udumavu.
Asilimia 12 wana ukondefu na asilimia tatu wana uzito pungufu huku akisema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uelewa mdogo wa masuala ya lishe.
“Mtoto hula shuleni lakini pia hula nyumbani. Tukimuelimisha mzazi, tunakuwa tumemsaidia mtoto moja kwa moja. Lishe bora ni msingi wa afya na maendeleo ya mtoto,” amesema Dk Mkuba.
Ameongeza kuwa lishe bora kwa mtoto wa kike kuanzia balehe ni muhimu katika ukuaji wa mwili, hususan nyonga, jambo linaloweza kuathiri hata uzazi baadaye.
“Kama mtoto wa kike hatapata chakula chenye virutubishi vinavyohitajika, ukuaji wa nyonga unaweza kuwa hafifu na baadaye akakabiliwa na changamoto wakati wa kujifungua. Lakini akipata lishe bora katika kipindi cha balehe, anaweza kuepuka matatizo hayo,” amesema.
Dk Mkuba amesisitiza kuwa lishe bora haipaswi kuangaliwa katika miaka ya awali pekee, bali iendelee hadi ujana, kwa sababu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya mwili, akili na ustawi wa kijamii.
Amesema vijana waliopata lishe bora huwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kubuni na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Tunapotunza lishe ya watoto wetu, tunaweka msingi wa taifa lenye nguvu. Vijana wenye afya njema na akili timamu watakuwa wataalamu, wabunifu na viongozi wa kesho,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe Mtafiti wa TFNC, Eliasaphi Mwana amesema kuimarishwa kwa mpango wa chakula shuleni kunalenga kukabiliana na hali ya lishe duni miongoni mwa watoto wa shule za msingi.
Wazazi walioshiriki mafunzo ya lishe bora yaliyotolewa na Taasisi ya lishe na chakula Tanzania yaliyofanyika katika shule ya msingi Likwati, wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Amesema utafiti wa mwaka 2019 (School Malaria and Nutrition) unaonyesha mtoto mmoja kati ya wanne katika shule za msingi anakabiliwa na udumavu, huku mtoto mmoja kati ya watatu akiwa na upungufu wa damu.
“Hali hii inatokana na changamoto za lishe shuleni na nyumbani, jambo linaloathiri ukuaji wa watoto na uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika masomo,” amesema Mwana.
Amesema watoto wanapokosa chakula cha kutosha wanapokuwa shuleni, usikivu na uelewa wao hupungua, hali inayosababisha kushuka kwa matokeo ya kitaaluma.
“Lishe shuleni si suala la chakula pekee, bali ni msingi wa mafanikio ya kielimu na maendeleo ya watoto. Tunawahimiza wazazi kushirikiana na shule na kamati za chakula kuhakikisha watoto wanapata milo kamili,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wazazi waliopata mafunzo hayo, Issa Komba amesema yamewasaidia kuelewa sababu zinazoweza kuchangia watoto kushindwa kuelewa masomo darasani.
“Tumepata elimu muhimu kwa ajili ya watoto wetu. Wazazi ambao hawakuhudhuria wanapaswa kuelimishwa pia. Ni vyema wawezeshaji wakatoa vipeperushi ili tuweze kufuatilia kwa urahisi kutokana na majukumu tuliyonayo,” amesema Komba.
Naye Ofisa Lishe wa Wilaya ya Temeke, Happu Mkunda amesema wameanzisha utaratibu wa kuwa na siku ya lishe kila robo ya mwaka ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi katika mitaa na vituo vya afya.
“Lengo ni kuhakikisha jamii inapata elimu ya lishe kwa wakati. Watoto wanapokuwa shuleni bila chakula cha kutosha, usikivu wao hupungua na matokeo yao hushuka. Hivyo, tunasisitiza ushiriki wa wazazi katika mpango wa chakula shuleni,” amesema Mkunda.