Dar es Salaam. Shahidi wa nne wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema kuwa alichokisikia Lissu akikitamka kwenye picha jongefu (video), ndicho kilichotokea siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.
Shahidi huyo ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri (waliopewa ulinzi, yaani wasiotakiwa kuonekana wala kutambulika), ametambulishwa kwa jina la P5 (33).
Shahidi huyo ametoa ushahidi wake akiwa ndani ya kizimba maalumu ambacho hakiwezeshi yeye kuonekana kwa wasikilizaji wala mshtakiwa isipokuwa kwa majaji tu.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika mwendelezo wa ushahidi wa Jamhuri, shahidi huyo wa nne katika ushahidi wake leo Alhamisi, Februari 12, 2026 akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli, amedai kuwa, anaishi Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na anafanya kazi ya ujasiriamali wa kuuza bidhaa za mkononi hususan viatu na soksi, anazozipata katika Soko la Ilala Boma na kuzitembeza katika maeneo ya Mchikichini, Posta Mpya mpaka Feri na wakati mwingine anaosha magari.
Amedai kuwa, Aprili 4, 2025 alikuwa maeneo ya Posta akiwa amejipumzisha kwenye bustani karibu na Benki ya NBC alikuwa anadurusu (peruse) katika mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp na Youtube kwa kutumia simu yake aina ya Smartphone Sony Experia.
Amedai kuwa, katika kudurusu huko mtandao wa Facebook aliona video ikimuonesha Tundu Lissu, anayemfahamu kupitia vyombo vya habari na mitandao kuwa ni mwanasiasa.
Shahidi huyo amedai kuwa, aliifungua video hiyo ili kusikia anasema nini, alimsikia akisema kuwa atahakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wa madiwani wabunge na Rais hautafanyika atahakikisha anakinukisha.
Pia, amedai kuwa, alimsikia Lissu akisema kuwa, polisi wanatumika kuiba kura na kwamba majaji nao ni ma-CCM hawatendi haki.
Amedai kuwa, katika video hiyo Lissu alikuwa amevalia Gwanda na tshirt nyeusi ndani akiwa jukwaani na nyuma yake kulikuwa na Bendera ya Taifa.
Amedai kuwa, baada ya hapo aliendelea kudurusu katika mitandao mbalimbali kisha akaelekea kituo cha daladala akapanda daladala kurudi nyumbani.
Amedai kuwa, aliposhuka kituoni alielekea maskani, kijiwe cha kahawa, ambako alikuta mzozo kuhusu ile video ya Lissu aliyoiona na kila mmoja akitoa hoja zake.
Amedai kuwa, wengi walikuwa wakimuunga mkono wa kukinukisha na kwamba watahakikisha siku ya uchaguzi watu hawaendi kupiga kura.
Amedai kuwa, kutokana na mzozo ule, aliona kutakuwa na vurugu siku ya uchaguzi na kwamba amani itavunjika kwa wao wafanyabiashara wanaotembea mtaani watashindwa kupata kipato na kufa njaa.
Amedai kuwa, alitoka kijiweni hapo akaenda nyumbani, lakini aliingiwa na woga.Yale maneno kukinukisha ndio yalimtisha akaona kuwa kutakuwa na uvunjifu wa amani.
Amedai kuwa, alimpigia simu ndugu yake ambaye ni askari polisi, Kituo cha Tabata Relini kumuuliza kama naye alikuwa amesikia hizo habari za Tundu Lissu, akamjibu kuwa wamezisikia na wanazifuatilia kuzifanyia kazi na akamtaka asiwe na wasiwasi.
Amedai kuwa, Aprili 9, 2025 asubuhi akiwa nyumbani alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni askari polisi akamtaka afike Kituo Kikuu cha Polisi (Central).
Amedai kuwa, alikwenda kituoni hapo alipofika alimpigia simu huyo askari, wakaonana akamchukua maelezo kwa mahojiano akamhoji kuhusiana na video hiyo.
Amedai kuwa, kile alichokisema kwenye video ile kukinukisha ndicho kilichotokea siku ya uchaguzi. Alikaa ndani siku sita.
Baada kumaliza ushahidi wake huo mkuu, shahidi huyo alihojiwa maswali ya dodoso na mshtakiwa Lissu anayejiwakilisha mwenyewe. Sehemu mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:
Lissu: Kwa hiyo huo ndio ushahidi ulioniweka gerezani miezi 10? Ameanza kwa kuhoji Lissu, akitabasamu na kuibua vicheko kwa wasikilizaji.
Jaji Ndunguru: Mshtakiwa twende kwenye maswali, uliza maswali
Lissu: Uliandika maelezo polisi siku ya Aprili 9, 2025?
Lissu: Ukioneshwa utayatambua?
Lissu ameomba shahidi apewe maelezo yake ayaangalie kama anayatambua na shahidi akakubali kuwa ndio maelezo yake na kwamba yana saini yake.
Lissu anasoma maelezo hayo kisha akaainisha maelezo ya ushahidi wa shahidi huyo alioutoa kizimbani ambayo hayako kwenye maelezo yake ya onyo aliyoyatoa polisi.
Baada ya kuanisha maelezo hayo alimuuliza shahidi huyo kama anapenda kuyatoa maelezo hayo mahakamani yawe kielelezo naye akakubali.
Upande wa mashtaka umeieleza Mahakama hauna pingamizi maelezo hayo ya shahidi wao kupokewa kuwa kielelezo cha mshtakiwa, hivyo Mahakama imeyapokea na kuwa kielelezo cha 3 cha upande wa utetezi (D3), kisha Lissu akamhoji maswali mbalimbali.
Lissu: Waeleze waheshimiwa kama kuna hayo maneno kwenye maelezo yako.
Lissu: Hebu naomba unioneshe mahali unakosema huwa unapata bidhaa zako Ilala Boma sokoni.
Lissu: Waeleze yapo hayapo? Natumaini wewe ni mwanaume.
Jaji Ndunguru: Naomba tuendelee
Lissu: Nasubiri jibu mheshimiwa, au amesemaje?
Jaji: Umesikia swali lake.
Shahidi: Sijaelewa swali rudia tena.
Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kuna maneno ulikuwa unapekua mitandao ya Whatsapp na Youtube; Facebook ipo.
Lissu: Hebu tuoneshe yalipo Youtube na Facebook.
Shahidi: Hapana, haikuandikwa.
Lissu: Uliulizwa kuhusu simu yako ukasema ulikuwa na Sony Experia Galaxy, kwenye maelezo yako yapo au hayapo?
Lissu: Waoneshe waheshimiwa majaji, yapo kwenye mstari wa ngapi?
Lissu: Soma twende pamoja na mimi nasoma huku.
Lissu: Hata kama uko kwenye kiboksi (kizimba kinachomfanya asionekane) utasoma tu.
Lissu: Hayapo, kweli si kweli?
Shahidi: Hayapo, vicheko.
Lissu: Katika maelezo yako yote hakuna mahali ambako unasema ulikuwa na simu, kweli si kweli?
Shahidi: Nilikuwa na simu lakini.
Lissu: Imeelezwa kwenye maelezo yako?
Lissu: Uliulizwa ukasema ulikuwa na akaunti ya Facebook, kwenye hayo maelezo yako iko?
Lissu: Shahidi, hayo maneno kwamba una akaunti ya Facebook, hayapo, siyo?
Shahidi: Yapo kwa sababu nimeyatolea ushahidi.
Lissu: Wewe una akili timamu?
Lissu: Hilo swali halijibiki, eeh… maneno kwamba ulikuwa na bando yako kwenye maelezo yako?
Shahidi: Yapo kwa sababu niliyatolea ushahidi.
Lissu: Mhemiwa Jaji sitaweza kuendelea maana shahidi hataki
Jaji Ndunguru anamfafanulia anamtaka shahidi ajibu maswali kulingana na anavyosilizwa.
Lissu: Ieleze Mahakama, maneno kwamba unamfahamu Tundu Lissu kama mwanasiasa kupitia vyombo vya habari na mitandao yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi: Hayapo lakini nitayatolea maelezo.
Lissu. Ndio maana nimeuliza kama una akili timamu, kwa hiyo ndivyo walivyokwambia nenda useme tu, wamekuuza?
Lissu: Umesema uliiona hiyo video, umewaonesha majaji maana hawajaiona.
Shahidi: Sijawaonesha maana simu iliharibika.
Lissu: Ulisema maneno mengi uliyoyasikia kwenye video, kwamba tutakinukisha, maana yake nini?
Shahidi: Kwamba ni kwenda kuchochea vurugu.
Lissu: Hiyo tafsiri umeitoa wapi?
Lissu: Mimi nina kamusi ngoja nikusomee maana yake… ni kutoa harufu mbaya) kuvunda na kunukia ni kutoa harufu nzuri, wewe hiyo tafsiri kwamba ni kuchochea vurugu umeitoa wapi?
Kesho hiyo inaendelea kwa shahidi wa tano kutoa ushahidi wake.