ACT Pemba watoa baraka  mazungumzo kujiunga SUK

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman akisema  kuwa mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar yanaendelea vizuri, wanachama wa chama hicho kutoka Pemba wamesema wako tayari kupokea uamuzi wowote utakaofikiwa katika mchakato huo.

Akizungumza na viongozi na wanachama wa ACT – Wazalendo Mkoa wa Kusini Pemba jana Jumatano Februari 11, 2026, Othman alisema mazungumzo kati ya chama chake na Chama cha Mapinduzi (CCM) yamefikia hatua muhimu.

Amewahakikishia wananchi kuwa taarifa rasmi itatolewa baada ya utaratibu wa ndani kukamilika.

Mazungumzo hayo yanaongozwa na Othman pamoja na mwenyekiti mstaafu wa ACT – Wazalendo, Juma Duni Haji huku upande wa CCM, ukiongozwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Amani Abeid Karume. Lengo ni kufikia mwafaka wa kudumu wa kisiasa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.




Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa ACT – Wazalendo Pemba, Mratibu wa chama hicho kisiwani humo, Rashid Ali Abdallah amemwahidi mwenyekiti huyo kuwa wanachama wana imani na uongozi wa chama na wako tayari kupokea uamuzi utakaofikiwa.

Abdallah ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 12, 2026, katika kikao cha ndani kilichofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Othman ya kukutana na wanachama na viongozi wa chama iliyoanza jana Jumatano.

“Mwenyekiti, sisi wanachama hatuna shaka na wewe na viongozi wenzako. Tuko tayari kupokea uamuzi wowote mtakaotuletea,” amesema Abdallah.

Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Mkoa wa Kichama wa Wete, Juma Khamis Ali ‘Kabakaba’ ameunga mkono kauli hiyo akisema wanachama wa mkoa huo wana imani na uamuzi utakaofanywa na viongozi wa kitaifa.

“Tunaelewa viongozi wetu ni wazalendo wanaojali masilahi ya Zanzibar na wananchi wake. Hatuoni sababu ya kuwa na shaka kuhusu mtakachoafikiana katika vikao,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema imani wanayoionesha wanachama kwa viongozi wao, ndiyo inayokifanya chama hicho kuendelea kuwa imara.

Akizungumza katika mkutano huo, Othman amesisitiza umuhimu wa Wazanzibari kuwa wamoja bila kujali tofauti za vyama vya siasa. Amesema migogoro ya kisiasa hutoa mwanya kwa watu wenye masilahi binafsi kuingilia mambo ya nchi, hivyo amehimiza mshikamano kwa ustawi wa Taifa.

“Lazima Wazanzibari tuwe kitu kimoja na tulinde nchi yetu ili adui asipate nafasi,” amesema.


Kwa mujibu wa Othman, mazungumzo hayo yanalenga kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) itakayojenga mshikamano na kulinda masilahi ya wananchi.

Amefafanua kuwa pande zote zimekubaliana kurejea katika vyama vyao kukamilisha taratibu za ndani kabla ya kutoa taarifa ya pamoja. Aidha, ameahidi kuwa makubaliano yatakayofikiwa yatarejesha imani ya wananchi kupitia utekelezaji wake kwa vitendo.

Othman ameongeza kuwa miongoni mwa masuala yaliyokubaliwa katika mazungumzo hayo ni kuimarisha mfumo wa uwajibikaji wa viongozi na kufanya mapitio ya mfumo wa uchaguzi ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.


Amesema pia kutakuwepo na utaratibu maalumu wa kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo mara baada ya taratibu za ndani za pande zote kukamilika.

“Tunataka Serikali ya Umoja wa Kitaifa iwe ya pamoja kweli, ili kila mmoja afurahie matunda yake. Kama mlivyoahidi, msiwe na hofu na viongozi wenu. Tuendelee kuwa pamoja ili tufanye mambo yetu kwa usalama,” amesema Othman.