Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limemuachia huru kiongozi wa madereva wa malori, mabasi na IT–Tanzania (Tatamata), Godlove Materu, aliyemshikilia kwa siku tano huku familia na umma wakikosa taarifa za kujua mahali alipo.
Wakati uongozi huo ukidai ameachiwa huru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga amethibitisha kwamba, “Ni kweli ameachiwa kwa dhamana na anatakiwa kuripoti kulingana na masharti aliyopewa,” amesema Kamanda Senga.
Materu alidaiwa kutekwa Februari 5, 2026 katika eneo la Chapwa, Tunduma mkoani Songwe, na watu watatu waliovaa kiraia, waliotumia gari aina ya Land Cruiser jeupe. Inadaiwa watu hao walijifanya wateja katika kibanda chake cha biashara ya vinywaji kabla ya kumchukua.
Baada ya viongozi wa Tatamata kuipa Serikali saa 48, wakitishia kusitisha huduma za usafirishaji endapo kiongozi wao asingepatikana, Jeshi la Polisi lilithibitisha kumshikilia kwa mahojiano.
Jeshi hilo lilidai linamshikilia na linamchunguza kuhusiana na tuhuma za kupanga matukio ya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe.
Hata hivyo, jeshi hilo halikuweka wazi kituo alichokuwa anashikiliwa, hali iliyozua malalamiko kutoka kwa familia na umoja wa madereva. Viongozi hao walitoa tamko hadharani wakilitaka Jeshi la Polisi kubainisha aliko ili mwanasheria wake aweze kumpatia haki zake za kisheria.
Kwa mujibu wa barua kwa umma iliyotolewa leo Februari 12, 2026 na wakili wake kutoka kampuni ya Haki Kwanza, Aloyce Komba, Materu aliachiwa Februari 9, 2026 baada ya kudhaminiwa na mke wake.
Kwa mujibu wa wakili huyo, Materu anatakiwa kuripoti kesho, Ijumaa Februari 13, 2026 saa 5 asubuhi, kwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Songwe, John Maro.
Komba amesema hadi wanatoa taarifa hiyo, mteja wake hakuwa amepewa maelezo rasmi kuhusu kosa au makosa ya jinai yanayomkabili katika kipindi chote alichoshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi, mikoa ya Songwe na Mbeya.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi bado linashikilia mali za Materu, zikiwemo kompyuta mpakato, simu mbili za mkononi pamoja na ufunguo na kufuli za kibanda chake cha biashara kilichopo mtaa wa Chapwa, Tunduma.
Akijibu madai hayo, Kamanda Senga amesema mtu hawezi kukamatwa na kuingizwa mahabusu bila kosa, lazima kuwe na jambo linalochunguzwa, ushahidi ukipatikana atapelekwa mahakamani.
“Kama hakuna ushahidi utapata dhamana au kesi inaishia hapo, hakuna anayekamatwa bila kosa na ukikamatwa lazima uambiwe kosa na lazima tuhuma zako ziwepo,” amesema.
Amesema kuna hatua ya kuandika maelezo baada ya kuelezwa tuhuma zinazomkabili “si kweli kwamba hana kosa na hajaambiwa kosa, ameshaambiwa,” amesema.
Ameongeza kuwa anatakiwa kuendelea kuripoti hadi upelelezi ukikamilika kulingana na siku alizopangiwa na ataambiwa nini kinafuata.