Go Green na Imbeju kuchagiza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema programu za Go Green na Imbeju zinaendana kikamilifu na malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa 2050.

Hiyo ni kutokana na kuweka mkazo katika uchumi jumuishi, shindani na himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi huku ikitambua vijana kama msingi wa kufikia mafanikio hayo.

Profesa Kitila amesema hayo leo Februari 12, 2026 jijini Dodoma wakati CRDB Bank Foundation ikizindua rasmi programu ya Go Green na Imbeju hiyo jijini Dodoma.

Programu ya Go Green na Imbeju inalenga kuwawezesha vijana wenye miradi bunifu inayohusiana na kilimo himilivu, nishati safi na jadidifu, teknolojia za maji, usimamizi wa taka, uhifadhi wa mazingira na ubunifu wa kidijitali kwa mitaji nafuu kuanzia Sh500,000 hadi Sh50 milioni.

Profesa Mkumbo amesema Serikali imekuwa ikiweka mkazo katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kukuza uchumi wa kijani na kujenga mifumo imara ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Miradi ya vijana inayolinda mazingira kama tunavyoiona leo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa Dira ya Taifa 2050 kwa vitendo,” amesema Profesa Mkumbo.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (katikati) akiwa na viongozi wengine wa wa Serikali, Bunge na Benki ya CRDB wakipata maelezo kutoka mwanzilishi wa kampuni ya Aquafresh iliyoshiriki katika maonesho ya biashara changa bunifu za vijana katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Go Green Na IMBEJU jijini Dodoma, leo Februari 12,2026. 



Amesema ushiriki wa sekta binafsi kwenye utekelezaji wa Dira 2050 ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mawazo bunifu ya vijana yanageuzwa kuwa biashara endelevu zenye ajira na tija kwa Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mpango huo ni daraja kati ya fedha za kimataifa za tabianchi na vijana wabunifu ambao mara nyingi hukosa dhamana au historia ya mikopo inayohitajika katika mifumo ya kawaida ya kifedha.

“Kupitia Go Green na Imbeju tunaamini vijana wengi zaidi watafikiwa, kuandaliwa na kuwezeshwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani. Huu ni muunganiko wa kimkakati kati ya ufadhili wa kimataifa wa tabianchi na ubunifu wa vijana wa Tanzania,” amesema Nsekela.

Ameeleza kuwa, kupitia programu ya TACATDP yenye thamani ya Dola 200 milioni za Marekani kwa ushirikiano na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UN GCF), tayari zaidi ya Sh100 bilioni zimetolewa kuwafikia takribani wanufaika 600,000 kote nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa ameeleza kwa kina mchakato wa utekelezaji wa programu hiyo na kubainisha kuwa imeundwa mahsusi kwa ajili ya vijana huku akisema mchakato wa maombi utafanyika kidijitali kupitia jukwaa la FursaHub kwa kushirikiana na NEDC.

“Maombi ya Go Green na Imbeju yatafanyika kidijitali kupitia mfumo wa Fursa Hub kuanzia Februari 12 hadi Machi 11, 2026. Mfumo huo utachuja maombi kulingana na vigezo vilivyowekwa, na yale yatakayokidhi masharti yatawasilishwa kwenye kamati ya wataalamu kwa tathmini ya kina ya uwezo wa biashara kujiendesha na kurejesha mitaji wezeshi yenye masharti nafuu,” amesema Mwambapa.

Baada ya hatua ya kwanza, waombaji watakaopita hatua hiyo wataalikwa kushiriki mafunzo maalumu ya biashara na ubunifu kupitia katika Kituo cha Ubunifu cha CRDB Bank Foundation kabla ya kupewa uwezeshaji wa kifedha.

“Kupitia dirisha hili tunatoa mitaji nafuu kuanzia Sh500,000 hadi Sh500 milioni kulingana na ukubwa na mahitaji ya mradi. Kwa miradi itakayofanya vizuri zaidi, kutakuwa na fursa ya kupata ruzuku ya kati ya Sh500,000 hadi Sh10 milioni kwa ajili ya kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara,” amesema Mwambapa.

Amesema tangu kuanzishwa kwa CRDB Bank Foundation mwaka 2023, zaidi ya wajasiriamali 1,250,000 wamefikiwa kupitia elimu ya fedha, mafunzo na mitaji wezeshi yenye thamani ya zaidi ya Sh21 bilioni, huku lengo likiwa kujenga mnyororo wa thamani unaowaandaa vijana kuingia katika mifumo rasmi ya kifedha.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo amesema Bunge limeweka msingi imara wa kisheria unaowezesha ulinzi wa mazingira na kukuza uchumi wa kijani, na kwamba programu hiyo ni mfano halisi wa kuunganisha sera, mitaji na ubunifu wa vijana.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (wapili kushoto) akiwasili katika  katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Go Green na IMBEJU inayolenga kuwezesha biashara na bunifu za kijani za vijana kama sehemu ya kuchochea uchumi wa kijani kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Alioongozana nao ni Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori (wapili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa.



Akizungumza kwa niaba ya biashara changa bunifu za vijana ambazo zilipata fursa ya kuonesha bunifu zao, Irene Vambi, mwanzilishi wa Mrembo Naturals, amesema kupitia programu ya Imbeju ameweza kupata mafunzo, ushauri wa kitaalamu na mitaji iliyomwezesha kupanua uzalishaji wa bidhaa zake za asili na kuongeza ajira kwa vijana wengine.

“Imbeju imenisaidia kubadilisha wazo langu kuwa biashara inayokua na kuajiri vijana wengine. Go Green na Imbeju ni fursa ya kweli kwa vijana wenye ubunifu na ndoto. Nawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii, waombe na wajiamini. Inawezekana kabisa,” amesema Vambi.