Profesa Msoffe ataka taka zitumike kuzalisha ajira

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter Msoffe amewataka wataalamu wa bioteknolojia kuangalia namna wanavyoweza kutumia fursa zinazoweza kupatikana katika takataka ili waweze kujiajiri.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina ya wadau wa bioteknolojia na mkutano wa mkuu wa mwaka wa chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST) uliofanyika leo Alhamisi, Februari 12, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema suala la kuamka kesho na kukuta kila mtu amepata ajira si jambo rahisi, lakini uwepo wa kazi za kufanya katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo na elimu ni vitu vinavyoweza kuleta matokeo chanya.

Amesema utambuzi wa kazi unaweza kutumiwa na vijana kutengeneza na kuvumbua mawazo yao ili waweze kubadili kazi kuwa ajira.

Alitaja takataka kuwa moja ya eneo lenye fursa nyingi ambalo likitumika vizuri linaweza kuzalisha ajira nyingi kama ilivyo kwa watu wanaotengeneza vyakula vya mifugo kwa kutumia funza, mbolea kwa taka ozo huku akisema ni eneo dogo lililotumika.

“Lakini taka zinaendelea kuzalishwa kila siku, kwani kila binadamu anachofanya anazalisha taka hivyo nawapa changamoto wataalamu wa bioteknolojia, angalieni namna ya kubadili fursa hizi kuwa kitu kinachoshikika mkononi kupitia udhibiti wa taka ngumu hasa katika majiji.”

“Kama tukiweza kuchakata hata asilimia 10 ya taka zinazozalishwa katika majiji zinaweza kuondoa vijana wengi katika hali ya kukosa kazi, wakajiajiri na kupata kipato,” amesema.

Mbali na hilo, amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira imejikita katika kushajihisha sekta binafsi ili iweze kuendelea kuwa injini ya uchumi.

Wakati Profesa Msoffe akiyasema hayo, ripoti ya Dar es Salaam Urban Resilience Project (DURP) ya Machi 13, 2024 inaonyesha kuwa asilimia 63.4 ya taka zinazozalishwa jijini Dar es Salaam ni zinazooza.

Taka hizo kwa kiasi kikubwa zinatokana na mabaki ya chakula na matunda, zinapooza hutoa gesijoto kama methane na kaboni, hivyo kuchochea mabadiliko ya tabianchi na mafuriko pale zinapoziba mifereji wakati wa mvua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 57 ya taka jijini Dar es Salaam huishia mitaani kati ya tani 5,300 zinazozalishwa kila siku, huku tani 1,500 pekee zikifikishwa dampo. Kati ya taka hizo, zaidi ya asilimia 60 ni zinazooza.

Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) inaonyesha tani bilioni 1.3 za chakula hupotea kila mwaka, na kuzalisha tani bilioni 3.3 za gesijoto, sawa na asilimia nane hadi 10 ya uzalishaji wa gesijoto duniani.

Akizungumzia kuhusu suala la mitaji inayoweza kutumiwa na wataalamu hao aliwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na Serikali ili waweze kutekeleza mawazo yao.

“Mwaka huu ndani ya siku 100 za uongozi wa Serikali ya awamu ya sita kuna fursa imetoka kuna Sh200 bilioni ambazo zinakwenda kuwasaidia vijana katika kufanya kazi zao za kiuchumi, sasa nyie ni miongoni mwao, fursa tayari imetolewa itumieni, tengenezeni mawazo yanayouzika ili muweze kupata fedha hizo,” amesema.

Mbali na hayo amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa ajili ya wataalamu wa bioteknolojia vyuoni.

Mwenyekiti wa BST,  Profesa Peter Msola alitaja kukosekana kwa ajira kama moja ya changamoto inayowakumba wataalamu wa fani hiyo jambo ambalo linafanya vijana kuhamia fani nyingine.

Pia alitaja uwepo wa miundombinu finyu katika vyuo na taasisi za utafiti ikiwemo maabara na vifaa vya maabara jambo ambalo linaathiri mafunzo kwa vitendo na ukuzaji wa ubunifu kwa vijana.

“Ukosefu wa mitaji ni kikwazo kingine kinachofanya vijana washindwe kufanya ubunifu, uanzishwaji wa Startups unahitaji mtaji mkubwa, wakati vijana wetu wanakosa fursa za mitaji ya uwekezaji na msaada wa kukuza biashara,” amesema.