……….. .
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki fursa za zabuni za serikali kupitia mfumo wa NeST, ikisisitiza kuwa zaidi ya shilingi trilioni tano zimetengwa mahsusi kwa ajili ya makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Akizungumza leo Februari 12, 2026 jijini Dodoma katika uzinduzi wa filamu ya Winga, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa PPRA, Remija Salvatory, amesema mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, hususan waliokuwa pembezoni, anapata taarifa na kushiriki kikamilifu katika fursa za ununuzi wa umma.
“Tunamkaribisha kila mmoja wenu awe balozi wa kuwajulisha Watanzania kwamba kupitia ununuzi wa umma kuna fursa za kufanya biashara na serikali.
Kuna fursa za kupata tenda za serikali na zipo fedha zilizotengwa moja kwa moja kwa ajili ya makundi maalum,” amesema Salvatory.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, taasisi zote za umma zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti zao kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Kiasi hicho kinakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi trilioni tano.
“Hii ni keki ya kila Mtanzania. Sisi kama mamlaka tuna hamu na hamasa kubwa kuhakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa wote,” amesisitiza.
Salvatory ameeleza kuwa PPRA imekuwa ikitoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, makongamano pamoja na kushirikiana na wasanii, lakini safari hii wameamua kutumia filamu kama jukwaa jipya la kufikisha ujumbe kwa makundi mapana zaidi.
“Tumekuja na filamu kwa sababu tunatambua kuna kundi linafuatilia zaidi tamthilia na filamu. Kupitia filamu ya Winga, watajifunza namna ya kufikia fursa hizi kwa njia rahisi na inayoeleweka,” amesema.
Amefafanua kuwa jina Winga limetumika kuashiria dhana ya “mtu wa kati”, akibainisha kuwa katika mfumo wa ununuzi wa umma kupitia NeST hakuna mtu wa kati.
“Kupitia mfumo wa NeST hakuna kitu kinachoitwa winga. NeST ndiyo muunganiko pekee wa tenda zote za serikali. Unachotakiwa ni kujisajili, kufuata taratibu na kuwasilisha maombi yako moja kwa moja. Hakuna dalali wala mtu wa kati,” ameeleza.
Ameongeza kuwa filamu hiyo itaonesha kwa vitendo namna zabuni zinavyotangazwa, jinsi ya kujisajili kwenye mfumo wa NeST na hatua za kufuata ili kushinda tenda kwa njia halali na ya uwazi.
PPRA imewahimiza Watanzania kuitazama filamu hiyo ili kupata elimu sahihi kuhusu mchakato wa zabuni za serikali na kuchangamkia fursa zilizopo, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kunufaika na rasilimali za umma.

