YANGA imetua jana kisiwani Zanzibar, tayari kwa mechi iliyoshikilia hatma ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, lakini kocha Pedro Goncalves ametoa kauli ya kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo juu ya ukosoaji wa kikosi hicho.
Aidha, bilionea wa klabu hiyo anatarajiwa kuwasapraizi wachezaji kwa kutinga uwanjani kuwapa sapoti katika pambano hilo la Kundi B litakalopigwa keshokutwa Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku.
Tuanze na kocha Pedro, akizungumza na Mwanaspoti amesema anafahamu kwamba mashabiki wa timu hiyo wameumizwa na matokeo ya kutoa sare nyumbani na kwenda kupoteza ugenini lakini wanafahamu sababu za kupoteza pointi hizo tano.
Pedro amesema hakuna mechi walioingia kwa hesabu za kujilinda zaidi kama ambavyo wengi wanaona, lakini makosa makubwa kwao ni kutotumia nafasi wanazozipata, jambo analolifanyia kazi kwa nguvu kwenye uwanja wa mazoezi.
“Wakati tunaanza mechi za makundi, kila mmoja alikuwa haoni nafasi yetu ya kwenda robo fainali na hili lilitokana na kuangukia kundi ambalo lina timu zenye rekodi kubwa Afrika na zilizofanya uwekezaji mkubwa,” amesema Pedro n kuongeza;
“Ukiangalia sasa ni tofauti kidogo ni vile tumefanya makosa ya kuangusha poiunti hizi tano kwa kutoa sare nyumbani na kupoteza ugenini, tulikuwa na nafasi kubwa kuondoa huu wasiwasi lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri hapa nyumbani katika mechi hiyo ya mwisho.”
Kocha huyo raia wa Ureno, amesema Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri dhidi ya Kabylie na kwamba wataingia uwanjani kutafuta ushindi kwa kuhakikisha wanatumia nafasi nyingi ambazo watazitengeneza.
Pedro alithibitisha washambuliaji wa timu hiyo wanapewa mazoezi mengi ya kuwaongezea utulivu, ili waweze kufanya kweli kuifungia mabao ya kutosha ili kumaliza kwa kishindo hatua ya makundi. “Nimeona watu wanasema ni kama tulikuwa tunajilinda sana lakini tunachukua maoni yao, ukweli ni kwamba hakuna mchezo tulioingia na hesabu hizo, tulitaka kushambulia lakini huwezi kuwa bora kwa mazingira ya mchezo uliopita,” amesema Pedro na kuongeza;
“Wakati mchezo unaanza tulikuwa vizuri bahati mbaya hali ilibadilika tukaanza kucheza mvua kubwa na upepo mkali unaoambatana na baridi kali niliona namna wachezaji walivyosumbuka, haikuwa hali ambayo tuliizoea tangu tulipofika pale, iliwasumbua wachezaji, tunaachana na hilo tunaangalia mchezo ujao.
“Tuna nafasi ya kurekebisha hilo hapa nyumbani, tutakwenda tena kushambulia kwa nguvu ili tupate mabao, tunafanya kazi kubwa ya kuwapa mazoezi tofauti wachezaji wetu ili waweze kuongeza utulivu wanapofika eneo la mwisho, tunahitaji mabao lakini pia tunatakiwa kuwa makini tusiruhusu hayo yote yanawezekana.”
Yanga inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao mawili huku wakiiombea Rabat ifungwe na Al Ahly.