HAKUNA kitu kinachosubiriwa kwa hamu na Wanayanga kwa sasa kama kuiona timu yao ikipata ushindi mbele ya JS Kabylie ya Algeria na kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kuna rekodi ya kutisha nyuma ya pambano hilo linalopigwa Jumapili.
Yanga inahitaji ushindi si chini ya mabao 2-0, huku ikiiombea mabaya AS FAR Rabat ya Morocco iteleze mbele ya Al Ahly ya Misri ili kukata tiketi ya robo fainali kwa mara pili ndani ya misimu mitatu ya michuano hiyo, jambo linalomfanya kocha Pedro Goncalves kukuna kichwa kwa sasa.
Licha ya mikakati na tambo zinazoendelea kwa wanayanga wakiamini watainyoa JS Kabylie na kutinga robo fainali, kuna rekodi ya kusisimua kwa Yanga dhidi ya klabu za kutoka Algeria ikiiweka mtegoni kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Hii ni mara ya nne kwa Yanga kukutana na timu kutoka Algeria katika mechi za kuamua hatma ya klabu hiyo katika michuano ya CAF, huku rekodi zikionyesha ni mara moja tu kati ya tatu za awali vijana wa Jangwani walitoboa mbele ya Waarabu hao wa Algeria.
Rekodi zinaonyesha ni mara moja tu, Yanga iliweza kufanya kweli na kutoboa mbele ya timu kutoka Algeria, lakini mbili nyingine ilichemsha na sasa inavaana tena na wapinzani wao hao wa Algeria wakiwa na hesabu za kutoingia mtegoni ili iweze kutinga robo fainali kwa mara nyingine.
Yanga ilitibuliwa na timu ya Algeria katika msimu wa 2022-2023 iliposhiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufika fainali.
Msimu huo ilivana na USM Alger na Yanga ilikuwa ikisaka heshima ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kubeba ubingwa wa Afrika kwa kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-1 kisha kwenda kushinda ugenini mjini Algiers na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.
Matokeo hayo yaliibeba zaidi USMA iliyokuwa chini ya kocha Abdelhak Benchikha kwani kanuni ya faida ya bao la ugenini iliwapa Waalgeria ubingwa huo wa Afrika mbele ya vijana wa Jangwani.
Msimu ulioifuata wa 2023-2024, Yanga ikisaka tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huo ilikuwa na kibarua cha kuvaana na CR Belouizdad ambayo iliwanyoa ugenini kwa mabao 3-0 na kulazimika kusaka ushindi wa mabao zaidi ya mabao hayo ili iwapiku Waarabu hao.
Yanga ikawashangaza CR Belouizdad kwa kuwafunga mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufanya matokeo ya jumla baina yao (h2h) kuwabeba Yanga mbele ya Waalgeria hao na kwenda robo licha y timu hizo kulingana pointi katika kundi lililokuwa pia na Al Ahly ya Misri.
Mabao ya yaliyofungwa na viungo Mudathir Yahya, Stephanie Aziz KI na washambuliaji Kennedy Musonda na Joseph Guede yalitosha kuivusha Yanga kwenda robo fainali, ikamaliza na pointi nane na kushika nafasi ya pili sawa na CR Belouizdad iliyokuwa ya tatu lakini kikosi hicho kikanufaika na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Mediama ya Ghana ikimaliza ya mwisho na pointi nne.
Msimu uliopita tena bahati ikawakutanisha Yanga na timu nyingine kutoka Algeria, MC Alger katika Kundi A, ambapo katika mechi ya mkondo wa kwanza ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 siku ya Desemba 7, 2024, wiki moja baada ya kulala 2-0 nyumbani katika mechi ya kwanza dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Mechi ya marudiano Yanga ikiwa nyumbani tena ikatakiwa kutafuta ushindi wowote ili ifuzu robo fainali na kila mwanayanga aliamini timu hiyo ingefanya kweli kwa kuwa inacheza Benjamin Mkapa, lakini Waalgeria hao waliwakatili kwa kukomaa na mechi kuisha kwa suluhu.
Matokeo hao yaliifanya Yanga ifikishe pointi nane na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Al Hilal iliyomaliza na pointi 10 ikiwa kinara wa kundi na MC Alger ikiwa ya pili ikikusanya pounti tisa nza zenyewe kufuzu robo fainali, huku Yanga na TP Mazembe ya DR Congo iliyomaliza mkiani na pointi tano zikiaga michuano hiyo.
Sasa kesho inakutana na JS Kabylie katika mazingira kama yale ya misimu mitatu mfululizo iliyopita ya kusaka matokeo mazuri ya kuamua hatma ya timu hiyo kuweka historia ikiwa tena nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Yanga inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao mawili, huku pia ikiiombea mabaya AS FAR Rabat ya Morocco ifungwe na Al Ahly ili kuirahisishia kazi ya kutinga robo fainali, vinginevyo safari itakuwa imeishia hapo.
Kwa sasa Al Ahly inaongozwa kundi B na kufuzu robo fainali mapema kwa kukusanya pointi tisa ikifuatiwa na FAR Rabat yenye nane, huku Yanga ikifuata na alama tano wakati JS Kabylie ikiwa na pointi mbili tu licha ya kila moja kucheza mechi tano hadi sasa.
Sare ya aina yoyote kule Cairo itaing’oa Yanga hata kama itashinda kwa idadi kubwa mbele ya JS Kabylie, kwani itaifanya Al Ahly kufikisha pointi 10 na FAR Rabat kufikisha tisa ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga. Lakini hata kama Al Ahly itashinda kwa mabao 4-0, kisha JS Kabylie ikakomaa kama ilivyokuwa mechi ya awali nyumbani iliyoisha kwa suluhu, vijana wa Pedro itakuwa kwaheri.
Jambo hilo limemfanya kocha Pedro kukiri kwamba mechi hizo za mwisho ni ngumu, lakini wao watapambana kuhakikisha wanapapata matokeo mazuri nyumbani baada ya kushindwa kuvuna pointi tatu mechi ya mwisho Amaan dhidi ya Al Ahly.