Barker anavyoanza upya Msimbazi, akitoa kauli nzito

BAADA ya Simba kushinda mabao 2-0 dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu, kocha wa timu hiyo Steve Barker, amesema ameanza kuyaona mabadiliko ya kikosi hicho na anaamini kitaendelea kuwa bora na cha ushindani mkali.

Katika mechi hiyo ya juzi usiku iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Simba ikiwa wageni mabao ya Wekundu hao yalifungwa na Seleman Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 37 na Libasse Gueye sekunde chache kabla ya mapumziko na kuipa pointi tatu na kuifanya ifikishe 19 kupitia mechi nane.

Barker amesema, wanaweka nguvu Ligi Kuu ambako wanaona wana nafasi ya kuwania taji hilo, kitu kinachomwaminisha ni mabadiliko ya wachezaji kurejesha ushindani anaoutarajia utakuwa endelevu dhidi ya timu pinzani.

“Naona mwanga wa Simba kuendelea kuwa bora siku hadi siku, hatuna nafasi Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kusalia na mechi moja ambayo tutapambania ushindi kwa ajili ya heshima ya klabu, ila nguvu kubwa kwa sasa itakuwa ligi ya ndani,” amesema Barker na kuongeza;

“Nafasi ya kupambania taji la ligi ya ndani ipo wazi, tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunarejesha imani kwa mashabiki kuifurahia timu ikishinda mechi na kuchukua mataji, natambua ina mashabiki wengi ambao wanaipenda klabu yao.”

Simba imepanda hadi nafasi ya tano kutoka ya saba, imefikisha pointi 19 katika mechi nane ilizocheza, imeshinda sita, sare moja na imefungwa mmoja, inamiliki mabao 16 imetikiswa nyavuni mara nne.

Kutokana na msimamo huo wa Ligi Kuu, kocha amesema ni suala la muda Simba kupanda nafasi za juu na kutimiza lengo la kuwania ubingwa: “Natambua ligi ni ngumu, lakini klabu ya Simba ni kubwa na wachezaji wanajua nini malengo yanayotakiwa.”

Misimu minne mfululizo iliyopita Simba imekuwa ikitoka kapa katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) kutokana na Yanga kutawala ikibeba misimu yote jambo ambalo Barker amesema ni nafasi ya kuweka mambo sawa licha ya kukiri ameiona Ligi yenye ushindani.

Kocha huo ataiongoza Simba kufunga hesabu za CAF katika mechi inayopigwa kesho kwene Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Stade Malien ya Mali iliyowatungua mabao 2-1 ugenini na kuchangia kuwazua Wekundu hao kuvuka kwenda makundi kutoka Kundi D.

Simba haijashinda mechi yoyote ya CAF msimu huu ikiwa nyumbani, kwani katika mechi nne zilizopita ilitoka sare tatu ikiwamo moja ya makundi na mbili za raundi za awali, huku ikipasuka moja kwa Petro Atletico ya Angola na mechi ya kesho ni ya kutafuta heshima mbele ya mashabiki.