Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, ametaja mambo mawili yatakayosaidia chama hicho kupata mwanga wa kufikiria kushiriki katika maridhiano yaliyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia alipofungua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, mjini Dodoma, kwenye hotuba yake alitangaza kuwa Serikali imeunda tume ya uchunguzi ili kubaini chanzo na mantiki ya vurugu za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Vurugu hizo zilisababisha vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali za umma na binafsi na kuliacha taifa katika mpasuko wa kisiasa na kijamii.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema tume hiyo itachunguza matukio hayo ili kubaini ukweli, kutoa mwanga kwa umma, na kuweka msingi wa mazungumzo, amani, na maridhiano ya kitaifa.
“Serikali ilinyoosha mkono kuwavuta na kuwakaribisha vyama vya siasa… mkono huo wa urahimu ulileta matumaini kwa nchi, kabla ya baadhi ya wadau kuamua kuuachilia au kuuputa mkono huo.
“Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano,” alifafanua Rais Samia kwenye hotuba yake bungeni.
Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Heche, ambaye ametaja mambo mawili yatakayotoa mwanga kwa chama hicho kufikiria kwenda kwenye maridhiano yaliyotangazwa na Rais Samia.
Mahojiano hayo yaliyofanyika Februari 10, 2026, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Heche amesema kuwa ili Chadema ifikirie kushiriki mazungumzo ya maridhiano, jambo la kwanza mwenyekiti wao, Tundu Lissu, aachiwe huru.
Amesema Lissu akiachiwa huru ndiye atakayeongoza vikao vya chama kujadili iwapo Chadema itaingia katika maridhiano hayo ama la.
“Kuachiwa Lissu ni moja, jambo la pili ni chama chetu kifunguliwe. Hapo ndiyo labda ajenda ya maridhiano inaweza kupelekwa kwenye vikao watu wakasema wanataka hicho kitu au hawakitaki,” amesema Heche.
Amesema kuwa katika suala hilo hakuna njia ya mkato itakayotumika kwa Chadema zaidi ya Lissu kuwa huru na chama hicho kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa bila vikwazo.
“Kitendo cha kumkamata mwenyekiti wetu na kumbambikia kesi ya uongo ni kuzuia hicho kitu hata kukifikiria kwamba tunaweza kuzungumza. Nasema hivyo kwa sababu mtu aliyechaguliwa Chadema ni Lissu, wengine wote ni wasaidizi wake, na uamuzi wowote utakaofanyika ndani ya chama ni kwa niaba yake na si vinginevyo,” amesema.
Heche ameonya kwamba mtu yoyote asijidanganye kwamba yeye (Heche) anaweza kuamua kitu ambacho ni kinyume na anachokifikiria Lissu.
“Mtu asije kujidanganya katika hili, mimi majukumu yangu ni kumsaidia yeye (Lissu) kutimiza malengo yake aliyowauzia wanachama nao wakamchagua kuwa mwenyekiti, na yeye ndiye mtu pekee atakayekiongoza chama kwenye maridhiano,” amesema.
Heche amesema hakuna njia ya mkato ndani ya chama hicho ya kushiriki kwenye maridhiano zaidi ya watu kukiri kuna makosa yametokea, wameumiza watu, na waliohusika wawajibishwe.
“Hakuna namna mtu anaweza kujifunza kwa mambo aliyoyafanya na asirudie bila hatua kuchukuliwa, nani ameteka watu, nani ameua watu na nani aliyeagiza haya yafanyike? Bila watu kuchukuliwa hatua mioyo ya walioumizwa haiwezi kupoa,” amesema.
Lissu yupo mahabusu kwa zaidi ya siku 300, anakabiliwa na kesi ya uhaini na kesi nyingine ya kutoa taarifa za uongo.
Alikamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuhitimisha mkutano wa kisiasa uliokuwa akieneza ujumbe wa Chadema wa “No Reforms, No Election” (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi), uliokuwa ukipigania marekebisho ya Katiba na mchakato wa uchaguzi.
Amri ya kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa ilitolewa Juni 10, 2025, na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, katika kesi ya madai ya mgawanyo sawa wa mali iliyofunguliwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kutoka upande wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa amri hiyo, Chadema hakiruhusiwi kuendesha mikutano ya kisiasa au shughuli nyingine za chama hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.
Mbali na mambo hayo, Heche amesema kuwa msingi wa maridhiano pia utajengwa kwa kuachiwa huru watu wote walioshikiliwa kwa masuala ya kisiasa, sambamba na familia za watu wanaotafuta ndugu zao waambiwe wako wapi au miili yao iko wapi. Pia, wote wanaotuhumiwa kuteka na kuua watu wawajibishwe.
“Hayo yakifanyika hapo ndipo Chadema tunaweza kusema chochote katika kwenda kwenye maridhiano,” amesema Heche.
Heche amesema kuna watu wanaofikiri kwamba Chadema si watu wanaopenda kumaliza mambo kwa mazungumzo, jambo ambalo si kweli.
“Huo ni uongo, mimi nimekuwa kwenye kamati iliyoitwa ya maridhiano. Chadema tulichaguliwa wawakilishi watano, nilikuwepo kwenye mazungumzo tangu Ikulu Chamwino (Dodoma), na tukawa hapa Dar es Salaam, mwaka mzima tunazungumza, kumbe ilikuwa ni uongo, hawakudhamiria hicho kitu,” amesema.
Amesema watu wengi huwa wanahoji masuala ya maridhiano, lakini swali la msingi, unakaa na nani katika hayo maridhiano?
“Chadema tunaweza kuridhiana na mtu aliyemkamata mwenyekiti wetu kwa kesi ambayo tunaamini ni ya uongo? Watu wanajua kwamba Lissu sio muaini, ni mwanasiasa anayefanya siasa zake kupingana na CCM (Chama cha Mapinduzi) na si vinginevyo,” amesema Heche.
Makamu mwenyekiti huyo wa Chadema amesema kuwa kama nchi imeamua kuingia katika mfumo wa siasa za vyama vingi, jambo la msingi ni kwamba kila chama kitambue na kuvumilia kuwepo kwa vyama vingine.
“Kila mwenye hoja tofauti aheshimu ya mwingine, hiyo ndiyo demokrasia. Maadamu tulikubali kuingia huko, basi tunahitaji kuvumiliana na kuwapa uhuru wananchi kuamua, lakini sio ilivyo kwetu ni kama vyama vingi imekuwa ni vita, wakati ilipaswa vitulete pamoja, lakini sasa vinatugawa,” amesema.
Heche amesema kuwa tangu mwaka 1992, nchi ilipoingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, ilipaswa kuwa imevuka hatua ya mgawanyiko wa kisiasa.
Amefafanua kwamba ukienda kinyume na misingi ya siasa za nchi, unaharibu uhusiano wa wananchi na kuleta mpasuko, lakini ukiendesha siasa vyema, unawaunganisha watu. Kwa hivyo, mfumo wa vyama vingi ulipaswa kuwaleta watu pamoja na si kuwagawa.
Akijibu maneno yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna watu wananufaika kisiasa na kifedha kwa sababu Lissu yupo ndani, Heche amesema kuwa ikiwa kuna hivyo, basi mwenyekiti wao aachiliwe ili watu hao wasiendelee kunufaika.
“Nimeona watu wanasema kuna watu wananufaika kisiasa na wengine kifedha Lissu kuwa ndani, nonsense (upuuzi). Mwenyekiti yupo ndani, hakuna mwanaharakati aliyefungua kesi hiyo, aliyeifungua anajulikana, wanaonufaika ni wao. Kama kuna mnufaika, basi wamuachie ili huyo mtu hayo manufaa hayapoteze,” amesema, na kuongeza;
“Wanajua Lissu hana nguvu yoyote ya fedha wala ya kimamlaka kupingana na nguvu zote za mamlaka, lakini wamemkamata, wamemuweka ndani, wamekamata viongozi wetu, wamefungua kesi kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa. Tunapitishwa kipindi kigumu, hata watu wetu wakienda mahakamani wanapigwa, wanavunjwa. Hayo maridhiano, katika hali hiyo, mnayafanya na nani?” amehoji Heche.
Chadema imehusika katika maridhiano kadhaa ya kisiasa kwa miongo kadhaa, hasa kama njia ya kupunguza mgogoro wa kisiasa na kudumisha amani.
Maridhiano ya vyama na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete (2012–2015), yalijulikana kama “Majadiliano ya kisiasa”. Lengo kupunguza mvutano wa kisiasa, kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki, na kuimarisha mshikamano wa taifa.
Maridhiano ya uchaguzi wa 2020: baada ya uchaguzi uliojaa malalamiko, Chadema ilihimiza mazungumzo kati ya vyama vyote vya upinzani na CCM. Lengo kupunguza vurugu, kulinda amani, na kuhakikisha mfumo wa vyama vingi unadumishwa.