Wiki iliyopita mstaafu alimalizia makala yake kwa kuandika, tufupishe; akiwa na maana ya kuitaka siri-kali na vibubu husika vifanye fasta kumlipa mstaafu wa kima cha chini shilingi milioni tano na laki tano zake walizoahidi wenyewe kumpa mstaafu… atakapokuwa mkazi wa Kinondoni na sio akiwa hai! Rukhsa wastaafu kucheka kwa uchungu!
Bila shaka mnakumbuka vibubu vilipoahidi kumpa mstaafu shilingi milioni tano na laki tano akiwa tayari amefariki na sio akiwa hai na tabu zake nyingi ikiwamo ile ya kila mwaka ya kulazimika kuhakikiwa! Hakika mstaafu anadhani kuwa wangekuwa wanalipwa pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi, nahisi tungekuwa tukihakikiwa kila wiki!
Mstaafu wetu anajikuta akijiuliza kama wale waheshimiwa na wenza wao wanaopokea pensheni ya mwezi ya shilingi kama anazopokea mstaafu kwenye pensheni yake ya miezi ishirini, wao nao wanahakikiwa kila mwaka au ni sisi tu kina ‘kananihii” nani! Ashakum si matusi.
Jumbe nyingi alizopokea mstaafu kutoka kwa wastaafu’ wenzie zimemtaka asifupishe maneno bali ayaongeze, wakiamini kuwa kuna mtu mahali siku moja atayasikiliza maumivu ya mstaafu wa kima cha chini na kuyachukulia hatua zinazopaswa! Siku haiko mbali
Hoja nyingi za wenzake zimemfanya mstaafu atafakakari sana hili la wastaafu’ kupewa wizara yao wenyewe wakati itatoka kwa siri-kali ile ile iliyowaweka miaka 21, rudia miaka, ishirini na moja kwa pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kabla ya Oktoba mwaka juzi kufanya kile walichosema wenyewe kuwa ni ‘kuboresha’ maisha ya mstaafu, kwa kumuongeza shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yake ya mwezi!
Mstaafu bado anajiuliza kama kwa siri-kali neno ‘kuboresha’ limekuwa na maana nyingine tofauti, linapomhusu mstaafu wa kima cha chini! Inaelekea hivyo.
Anashukuru sana kwamba hata siri-kali inaelekea imejiuliza upya na kuanzia Oktoba mwaka jana imeamua kumlipa mstaafu wetu nyongeza ya pensheni ya shilingi laki mbili na hamsini elfu kwa mwezi. Kumbe kila kitu kinawezekana, ni utashi tu! Mungu sio Athumani wala Chesi!
Wakati mstaafu wetu akiungoja tena utashi huu ufanye kazi tena na apate pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi ili aboreshe kweli maisha yake, anafikiria sana hili la wastaafu kuanzisha chama cha kuipigania haki yao kweli kabla ya kuwa wakazi wa kudumu wa Kinondoni !
Anawaza kuwa wastaafu wakija kupewa, wizara yao ya wastaafu’ bado itakuwa ni wizara moja ya siri – kali na wastaafu watabaki ‘kuboreshewa’ maisha yao vile vile vya baada ya miaka 21, kama kawaida!
Anajiuliza kuhusu kuunda chama cha kupigania haki za wastaafu na sio cha siasa ambayo kwao ‘si halisi.’ Miongoni mwa mengi yatakaofanywa na chama hicho ni kusimama kidete kuiuliza siri-kali na vibubu husika, hela zao walizokatwa kwenye mishahara kwa miaka 40 ya uajiriwa zimetumikaje na zinatumikaje! Ndio hii pensheni ya laki mbili unusu?
Kama zimetumika kujenga hivi vikwangua anga vya kukodisha vilivyoenea sasa nchi nzima, ni nani ‘baba mwenye nyumba’ anayeshika kodi na inaishia wapi, huku huyu mstaafu ndio kwanza, akiishia kulipwa kimya kimya shilingi laki mbili unusu kwa mwezi wakati kibubu kiliwawekea hela zao kwa miaka 40 ya ajira yao!
Na mstaafu anapotakiwa afe kwanza ndipo apewe shilingi milioni tano na laki tano zake, mbona kama mnamzingua tu? Kinazuia nini asipewe milioni tano na laki tano zake akiwa hai na akala jasho lake kwa amani?
Chama kitaweza kukihoji hiki kibubu? Kwa nini hakitayarishi mkutano mmoja japo mara moja kwa mwaka ili kujua matatizo ya wadau wake. Kitaweza pia kuhoji, hivi nyongeza ya pensheni anatoa siri-kali ama kibubu husika na ni nani anayepanga viwango vya pensheni ya wastaafu katie ya siri-kali na kibubu?
Huyu anafaa atafutwe ili atufahamishe jinsi anavyoamua hawa wapewe pensheni pamoja na wenza wao lakini hawa kina Chesi wagombanie laki mbili unusu na wenza wao ambao wahusika sasa wanajifanya hawawatambui! Kinondoni, usubiri kwanza tulifanyie kazi hili…!
0754 340606 / 0784 34p606