Makosa yanayofanywa na wafungaji Swaumu 

Dar es Salaam. Kujifunza Sharia za Swaumu na hukumu zake ni wajibu kwa Muislamu, ili afunge kwa namna anayopenda na kuiridhia Allah Mtukufu, na apate thawabu kamili na lengo lililokusudiwa, ambalo ni kumcha Allah Mtukufu.

Wapo wanaofunga lakini hawaufikii uchamungu, kwa ujinga wao wa kutojifunza sharia, masharti na adabu za Swaumu. Na wapo ambao inawalazimu kufungua kwa sababu ya ugonjwa hatari au udhuru wa kisharia, lakini wanaendelea kufunga na hivyo kuingia katika dhambi.

Kwa hiyo, kujifunza Sharia za Saumu na hukumu zake ni wajibu wa lazima kwa kila aliyewajbihswa kufunga.

Miongoni mwa makosa yanayofanywa na baadhi ya wafungaji wanawake na wanaume. Mosi: Baadhi ya Waislamu kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kupindukia katika kununua vyakula na vinywaji kwa wingi, badala ya kujiandaa kwa utiifu.

Pili. kuharakisha kula daku kwani Sunna ni kuwahi kufuturu na kuchelewesha kula daku.  Tatu, kuacha kutia nia ya kufunga usiku, Ramadhani inapoingia, ni wajibu kutia nia ya kufunga tangu usiku.

Mtume  wa Allah amesema: “Asiyetia nia ya kufunga usiku, basi hana saumu.” Nia mahali pake ni moyoni. Nne, kunywa kwa makusudi wakati wa adhana ya Alfajiri ya kweli, na kwa kufanya hivyo mtu huwa ameharibu saumu yake.

Tano, kutojua au kutozingatia fadhila ya Ramadhani, kiasi cha kuupokea kama miezi mingine ya mwaka. Mtume wa Allah amesema: “Ramadhani ikiingia, hufunguliwa milango ya pepo, hufungwa milango ya moto, na mashetani hutiwa pingu.”

Sita, baadhi ya watu hawaswali Tarawehe usiku wa kwanza wa Ramadhani. Hili ni kosa, kwani mara tu unapoonekana mwezi wa Ramadhani, Muislamu huwa tayari ameingia katika usiku wa kwanza wa Ramadhani.

Saba, baadhi ya wazazi kuwazuia mabinti zao kufunga wakidai kuwa ni wadogo. Sheikh Ibn Jibrin  (Allah Amrehemu) amesema: Wasichana wengi huanza kupata hedhi wakiwa na umri wa miaka kumi au kumi na moja; wazazi wao huwapuuzia wakidhani bado ni wadogo. Nane, miongoni mwa makosa ni mtu kujihisi na wasiwasi anapokumbuka kuwa alikula au alikunywa kwa kusahau wakati wa kufunga, akidhani kuwa saumu yake imeharibika. Mtume wa Allah amesema: “Anapokula au kunywa mmoja wenu kwa kusahau, basi akamilishe saumu yake, Allah Mtukufu ndiye aliyemlisha na kumnywesha.”

Tisa, kutia hina, wanja, dawa ya matone ya sikio, au matone ya macho; vyote hivyo havibatilishi saumu yake. Kumi, baadhi ya wanawake kuhofia kuonja chakula kwa kuogopa kuharibu saumu.

Sheikh Ibn Jibrin  (Allah Amrehemu) amesema: Hakuna ubaya kuonja chakula kwa haja, kwa kukiweka kwenye ncha ya ulimi ili kujua ladha yake, bila kumeza chochote, saumu yake haiharibiki.

Kumi na moja, miongoni mwa makosa makubwa ni ujinga wa baadhi ya watu kuhusu yanayoharibu saumu, hususan mwanzoni mwa Ramadhani.

Mengine ni kuhofia kutumia mswaki mchana wa Ramadhani kwa kudhani kuwa anaharibu saumu. Mtume amesema: “Lau si kuwaletea uzito umma wangu, ningewaamrisha watumie mswaki kila wanaposwali.”

Kuchelewesha adhana ya Magharibi kwa kisingizio cha tahadhari, baadhi ya waadhini kuchelewesha adhana ya Magharibi hadi giza lienee, wakidai kuwa hilo ni tahadhari zaidi katika ibada.

Hili linapingana na Sunna, kwani Sunna ni kuadhini mara tu jua linapozama kabisa. Miongoni mwa makosa ni kughafilika kuwaombea dua waliowaalika kufuturu. Miongoni mwa dua hizo ni: “Ewe Allah, wabariki ulichowaruzuku, uwasamehe na uwarehemu.”

Baadhi ya watu hudhani kuwa kujamiiana na wake zao usiku wa mwezi wa Ramadhani ni haramu. Hili ni kosa, kwani uharamu ni mchana tu, ama usiku ni halali..”

Baadhi ya wanawake kuacha kufunga iwapo damu ya hedhi imekatika kabla ya alfajiri lakini hawajaweza kuoga kwa sababu ya muda kuwa mfupi, wakidai kuwa alfajiri imewakuta bila kuoga.

Damu ya hedhi ikikatika wakati wa kuchomoza alfajiri au kabla yake kidogo, saumu yake ni sahihi.   Miongoni mwa makosa ni mtu kuamka na janaba asubuhi kisha kudhani saumu yake imeharibika na atalazimika kuilipa. Ukweli ni kwamba saumu yake ni sahihi.

Mtume alikuwa akipambazukiwa akiwa na janaba kisha huoga na kuendelea kufunga. Kadhalika kuota usingizini (unatokwa na shahawa) hakubatilishi saumu, kwa kuwa si kwa hiari ya mwenye kufunga hata ikiwa machana; anatakiwa tu kuoga janaba akiona manii).

Miongoni mwa makosa ni kuchelewesha kufuturu. Sunna ni kuharakisha kufuturu mara tu inapothibitika kuingia wakati. Mtume wa Allah amesema: “Harakisheni kufuturu, na chelewesheni kula daku.”

Kosa lingine ni kughafilika kuomba dua wakati wa kufungua, ilhali dua ya mwenye kufunga hairudishwi. Mtume wa Allah amesema: “Dua za watu wa aina  tatu hazirudishwi: dua ya mzazi, dua ya mwenye kufunga, na dua ya msafiri.” Na miongoni mwa dua sahihi ni kusema: “Kiu kimeondoka, mishipa imeloa, na thawabu zimethibiti, Allah akipenda.”